…………….
Na Farida Mangube. Morogoro
WAENDESHA mashtaka na wapelelezi juu ya upelelezi unaofanikisha mshtaka wa kutoka vyombo mbalimbali wametakiwa kufanya kazi zao kwa weledi wakijua ya kwamba adui wa kwanza katika kutoa haki ni rushwa.
Naibu Mkuu wa Chuo Mipango , Fedha na Utawala kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto , Profesa Fatihiya Massawe alisema hayo jana mjini Morogoro wakati akifunga mafunzo yaliyodumu kwa wiki mbili ya upelelezi unaofanikisha uendeshaji wa mashtaka wenye tija ili kuboresha upatikanaji wa haki jinai.
Profesa Massawe alisema kuwa jukumu la upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ni dhamana waliyopewa kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.
Hivyo aliwataka kuwajibika kutenda kazi zao kwa mujibu wa sheria , kanuni , taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo, bila kusahau kuweka mbali upendeleo au chuki katika uwajibikaji wao.
“ Niwakumbushe pia kuwa mfanye kazi zenu vizuri mkijua kuwa adui wa kwanza katika kutoa haki ni rushwa , hivyo muepuke rushwa kwa namna yoyote ile “ alisisitiza Profesa Massawe
Alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kupunguza na kumaliza kwa asilimia tano mashauri ya mlundikano yaliyopo Mahakamani yanayochelewa kusikilizwa kutokana na upelelezi kutokamilika kwa wakati ifikapo mwaka 2025.
“ Matarajio ya Mahakama ni makubwa juu ya kuongezeka kwa kasi ya kushughulikia mashauri kwa kukamilisha upelelezi kwa wakati na mtakuwa mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawajapata bahati ya kuhudhuria mafunzo haya” alisema Profesa Massawe
Akizungumzia matumizi ya Tehama , Profesa Massawe alisema kwa hivi sasa hatuwezi kukweka kuitumia , Tehama ni fursa ya maendeleo ambayo yanawezesha upatikanaji wa taarifa mbalimbali .
Profesa Massawe alisema kwa mfano , mahakama imewezesha maamuzi ya mahakama , sheria na miongozo mbalimbali kupatikana kwenye mtandao wa Tanzilii ( Tanzania Legal Information Institute).
Profesa Massawe alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho ya Mahakama ambayo yanatekelezwa kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano 2020/21- 2024/2025 na ni utekelezaji pia wa Sera ya Mafunzo ya Taifa 2003 pamoja na Sera ya Mafunzo ya Kimahakama 2019.
Washiriki 250 kutoka taasisi za Ofisi za Mashtaka, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya , Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa , Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania pamoja na Ofisi ya Kudhibiti Fedha Haramu ambao walipatiwa mafunzo hayo kwa awamu nne .
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania , Kanda ya Morogoro, Paul Ngwembe , Februari 27, mwaka huu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro na yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili wa Banki ya Dunia kupitia mradi wa Maboresho awamu ya pili.
Katika risala ya wahitimu iliyosomwa kwa niaba yao na Wakili wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Mashtaka , Sara Amandus, aliishukuru Mahakama ya Tanzania kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kutoa mafunzo hayo yaliyowajengea uelewa wa pamoja kwenye sheria , mbinu na taratibu za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka
Pia mafunzo hayo yametoa fursa kwao kubalilishana uzoefu kuhusu utendaji kazo wao wa kila siku ikiwemo changamoto zinazotokana na kukua kwa teknolojia na kubadilika kwa mbinu za uhalifu na wahalifu.