Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja akitoa taarifa kwa
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (wa pili kushoto)
kuhusu ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta Wilaya ya Ikungi mkoani Singida
wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi ya maendeleo aliyoifanya
Februari 28, 2023. 

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi
amesema moja ya mafanikio makubwa waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili
tangu aingie madarakani Rais Samia Suluhu Hassan ni ujenzi wa Chuo cha Ufundi
Stadi cha Veta na akatumia nafasi hiyo kuwapongeza Veta Kanda ya Kati kwa ujenzi
wa viwango vya hali ya  juu wa chuo hicho wilayani humo.

Kijazi alizungumza hayo mwishoni mwa wiki wakati wa utoaji wa taarifa ya
mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili tangia
aingie madarakani Rais Samia Suluhu Hassan na kumpongeza kwa mambo makubwa ya
maendeleo yaliyofanyika katika wilaya hiyo na mkoa wa Singida kwa ujumla.

Kijazi alisema ujenzi wa chuo hicho ni fahari kwa wilaya hiyo kwani kitaanza kutoa
mafunzo ya ufundi wa aina mbalimbali kwa vijana wa wilaya hiyo na za jirani jambo ambalo litawasaidia kujiajiri na kuajiriwa katika
maeneo tofauti kulingana na fani zao za ufundi watakazo kuwa wamejifunza.

“Tulikuwa na changamoto kubwa ya vijana wetu wanaomaliza elimu ya
msingi na sekondari kwenda kupata elimu ya ufundi nje ya wilaya yetu lakini
kukamilika kwa ujenzi wa chuo cha Veta hapa Ikungi kunakwenda kuondoa
changamoto hiyo,” alisema Kijazi.

Kijazi alisema anampongeza Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya
ujenzi wa chuo hicho ambacho kitakuwa mkombozi kwa wana Ikungi na wilaya jirani
ambacho kimejengwa na Veta Kanda ya Kati Dodoma.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya
Kati John Mwanja akizungumzia ujenzi wa chuo hicho alisema
Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi chenye umiliki wa Hati

namba: 2218- SGD  kimejengwa  katika 
Kijiji  cha Muungano,Kata  ya Unyahati 
wilayani  Ikungi  katika 
mkoa  wa Singida kwenye eneo lenye
ukubwa wa ekari 50.

Alisema Mradi huo  ulianza mnamo
mwezi Machi, 2020 ukisimamiwa na chuo cha VETA Singida na ulipaswa kutekelezwa
kwa muda wa miezi sita hata hivyo, haukuweza kukamilika kwa wakati kutokana na
changamoto kadhaa zilizojitokeza na baadaye mradi kusimama kwa muda wa mwaka
mmoja.

Alisema Mkurugenzi Mkuu wa VETA Februari 28/2022 alihamishia majukumu
ya usimamizi wa Ujenzi wa chuo hicho 
kutoka Chuo cha VETA Singida kwenda ofisi ya  Mkurugenzi wa VETA Kanda ya kati ambaye hadi
sasa ndiye anaendelea na usimamizi wa ujenzi huo ambao unatekelezwa kwa  mfumo wa “Force Account”.

Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi huo alisema unahusisha jumla ya
majengo 17 ambayo ni Jengo moja la utawala, Majengo manne  ya karakana, jengo moja la madarasa mawili
makubwa, majengo mawili  ya mabweni  (Wasichana na Wavulana), Bwalo la chakula na
Jiko, Majengo Matatu  ya vyoo (Wasichana
Wavulana  na  Watumishi), 
nyumba  mbili  (2) 
za  watumishi,  jengo 
la  umeme,  Jengo 
la  bohari  na kibanda cha mlinzi. Kwa wastani
hatua ya ujenzi hadi sasa imefikia asilimia 96%.

Alisema  chuo
kitakapokamilika, kitaendesha mafunzo ya kozi ndefu na fupi na kuwa ya muda
mrefu yatachukua muda wa miaka miwili hadi mitatu ambayo  yatatolewa katika fani zipatazo sita katika
awamu ya kwanza mara chuo kitakapokamilika ambazo ni Uhazili na Kompyuta (Secretarial
and Computer Application), Ushonaji (Design Sewing and Cloth Technology), Uashi
(Masonry and Bricklaying), Umeme wa Majumbani (Electrical Installation), Ufundi
Magari (Motor Vehicle Mechanics) na Uchomeleaji Vyuma (Welding and Metal
Fabrication). 

Alisema chuo  kitakuwa  na 
uwezo  wa  kudahili 
wanafunzi  240  wa 
kozi  ndefu  na 
uwezo  wa  kuchukua wanafunzi 144 wa bweni  (wasichana 64 na wavulana 80).

Alisema pia, kutakuwa na mafunzo ya muda mfupi (Short Courses)
yatakayochukua muda wa mwezi mmoja hadi miezi sita (6); kwa wastani mafunzo
hayo yanakadiriwa kudahili wanafunzi wapatao 250 hadi 900 kwa mwaka kutegemeana
na mahitaji ya jamii na shughuli za kiuchumi za eneo hilo.

  Mwanja, alisema ujenzi wa chuo hicho
ulianza katika bajeti ya 2019/2020 ambapo hadi sasa Sh.bilioni 2.3
zimeshatumika katika ujenzi huo ambao utakamilika Aprili mwaka huu.

Mwanja alisema Serikali imetoa Sh.milioni 259 ili kukamilisha ujenzi wa
chuo hicho na kwamba kitaanza kutoa mafunzo ya kozi ndefu kwa wanafunzi 240 na wa
kozi fupi kati wanafunzi 250 hadi 900 kwa mwaka.

Alisema faida ya chuo hicho mara kitakapokamilika kinatarajiwa kuhudumia
wakazi wapatao 343,985 wa Wilaya ya Ikungi na wakazi wapatao  1,754,370
wa Mkoa  wa  Singida.

Alisema katika kutekeleza mradi huo VETA imekumbana na changamoto mbali
mbali kama kupanda  kwa bei  ya
vifaa vya  ujenzi  wakati wakiendelea  na
utekelezaji wa  mradi,  hali iliyopelekea  pesa iliyotengwa  kutokidhi
mahitaji halisi  ya  mradi kutokana  na  bei
za  vifaa kupanda zaidi ya matarajio ya
awali.

Alitaja changamoto nyingine waliyokumbana nayo ni uwezo mdogo wa kiuchumi
wa mafundi waliowatumia hivyo kupelekea kushindwa kuwalipa vibarua wao kwa
wakati na kupelekea baadhi yao kuacha kazi, hivyo kupelekea kuchelewa kwa
utekelezaji wa mradi.

Mwanja alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu
ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha
mafunzo ya ufundi stadi nchini kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo
ujenzi wa vyuo vipya vya Veta na uboreshaji wa vyuo vya zamani na kuwa wao
wakiwa na dhamana ya kusimamia Veta wataendelea kuunga mkono jitihada za
Serikali na kuhakikisha Veta inakuwa juu siku zote kwa kutoa mafunzo bora na
sio bora mafunzo kwa mustakabari wa Taifa la Tanzania.