Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Maalum ya Kitaifa ya Kupambana na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa, Profesa Hezron Nonga, akifungua Kongamano la Kisayansi  la kujadili na kuwasilisha matokeo ya tafiti kuhusu usugu wa vimelea dhidi ya dawa lililofanyika Juni 3, 2026, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam.

Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Erasto Mbugi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano la Kisayansi   kuhusu usugu wa vimelea

Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Microbiology MUHAS, Lilian Kiwone akieleza umuhimu wa kushiriki Kongamano la Kisayansi   kuhusu usugu wa vimelea.

…………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeandaa Kongamano la Kisayansi linalolenga kujadili na kuwasilisha matokeo ya tafiti kuhusu usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa binadamu na wanyama pamoja na uhamasisha ufugaji wa kisasa unaozingatia usafi wa mazingira ya mifugo ili kupunguza hatari ya maambukizi yanayoweza kuchochea usugu wa vimelea.

Akifungua kongamano hilo jijini Dar es Salaam Juni 3, 2026, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Maalum ya Kitaifa ya Kupambana na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa, Profesa Hezron Nonga, amesema hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali, taasisi za elimu na wadau wa afya zimechangia kupungua kwa vifo vinavyohusishwa na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

Amesema jamii inapaswa kuendelea kupewa elimu kuhusu hali ya usugu wa vimelea katika afya ya binadamu na mifugo, huku akibainisha kuwa matumizi holela ya dawa za antibiotiki yamepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo ambalo limechangia kudhibiti ongezeko la usugu huo.

Profesa Nonga, kutoka Sokoine University of Agriculture (SUA), amesema kamati hiyo inaendelea kuratibu juhudi za kitaifa za kukabiliana na changamoto ya usugu wa vimelea, hasa dhidi ya dawa za antibiotiki.

Ameongeza kuwa ushiriki wa vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta binafsi unaimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo ambalo linaendelea kuwa tishio kwa afya ya umma.

“Usugu wa vimelea dhidi ya dawa bado upo na unaendelea kuongezeka, ndiyo sababu kulianzishwa kamati maalum ya kitaifa ili kuratibu juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo,” amesema Profesa Nonga.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Erasto Mbugi, amesema chuo hicho kina jukumu la kufundisha, kufanya tafiti na kutoa huduma za afya, hivyo kina nafasi muhimu katika mapambano dhidi ya usugu wa vimelea.

Amesema kongamano hilo limebeba agenda muhimu ya kuwajengea wanafunzi na wataalamu wa afya uelewa mpana kuhusu athari za usugu wa vimelea, hasa katika matibabu ya magonjwa ya kuambukiza.

Profesa Mbugi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuandaa warsha na mafunzo kwa wataalamu wa afya ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya dawa, sambamba na kuimarisha tafiti zitakazosaidia kubaini mbinu mpya za matibabu na dawa zenye uwezo wa kukabiliana na vimelea sugu.

Ameeleza kuwa kongamano hilo linatoa fursa kwa watoa huduma za afya, watafiti na wanafunzi kubadilishana uzoefu, kujifunza matokeo ya tafiti mbalimbali na kujenga uwezo wa pamoja katika kudhibiti tatizo hilo.

Naye mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Microbiology MUHAS, Lilian Kiwone, amesema kongamano hilo limewapa wanafunzi nafasi ya kuelewa kwa kina ukubwa wa changamoto ya usugu wa vimelea na mchango unaohitajika kutoka kwa wanasayansi katika kuitafutia suluhisho.

Amesema maarifa yanayotolewa kupitia tafiti mbalimbali zinazowasilishwa yatawawezesha wanafunzi kufanya tafiti zenye tija, kuelimisha jamii na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza kasi ya kuenea kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

“Tumepata uelewa mpana zaidi kuhusu namna ambavyo sisi kama wanafunzi na watafiti wa baadaye tunaweza kushiriki katika kuisaidia jamii kudhibiti usugu wa vimelea dhidi ya dawa,” amesema Kiwone.