Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa , Mwalimu wa panya wanaonusa na kubaini mate au makohozi yenye vijidudu vya ugonjwa wa Kifua Kikuu, Mariam Chamkwata wa Chuo Kikuu cha Kilimo, Sokoine cha Morogoro, katika maonyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, Machi 24, 2023. Wa pili kulia ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteremka kutoka kwenye gari lenye maabara inayotumika kupima ugonjwa wa Kifua Kikuu katika maeneo mbalimbali wakati alipotembelea mabanda ya monyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye uwanja a Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, Machi 23, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Na. WAF – Simiyu, Bariadi
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa amesema kuwa vifo vinavyosababishwa na Kifua Kikuu vimepungua kutoka vifo 55,000 vilivyotokea mwaka 2015 hadi vifo 25,800 sawa na asilimia 55% kwa Tanzania.
Hayo ameyasema leo Machi 24, 2023 kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2022 kwenye Maadhimisho Siku ya Kifua Kikuu Duniani ambapo Kitaifa yamefanyika katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
“Halikadhalika tumepunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu kutoka kiwango cha wagonjwa 306 katika kila idadi ya watu 100,000 kufikia wagonjwa 208 katika kila watu 100,000 ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 32.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha kuwa ugojwa wa Kifua Kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria ambao unaambukizwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa wa Kifua Kikuu ambaye hajaanza matibabu kwenda kwa mtu mwingine.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 87 ya wagonjwa wote duniani.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa
Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa Pamoja na ukubwa huu wa tatizo hili, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi na kuwekeza katika huduma za Kifua Kikuu ikiwemo kuongeza wigo wa huduma ili kuwafikia wananchi hususani katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya ugonjwa huu hapa nchini.
Hata hivyo, Wazri Mkuu Majaliwa amesema Ifahamike kuwa Kifua Kikuu ni ugonjwa mtambuka ambao sekta ya afya pekee haitoshi kutokomeza, hivyo ni budi kuweka mkakati wa kitaifa utakaowezesha ushiriki wa sekta nyingine katika kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa waathirika zaidi wa ugonjwa wa Kifua Kikuu ni watu wa hali ya kipato cha chini.
“Nawaomba sana tuchukue tahadhari juu ya ugonjwa lakini huu lakini pia tuwahi katika vituo vya huduma za afya na tutoe taarifa kama unahisi mtu anaugonjwa huu kwakua ugonjwa huu ni hatari sana.” amesema Waziri Ummy
Pia, Waziri Ummy amesema ugonjwa wa Kifua Kikuu unatibika endapo mgonjwa atawahi kituo cha kutoa huduma za afya kwa wakati na kupata matibabu.
Waziri Ummy amesema kupitia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara imejitahidi kuhakikisha huduma bora zinatolewa pamoja na Dawa zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mwisho Waziri Ummy ametoa wito kwa Watanzania wote wenye dalili za Kifua Kikuu kwenda kwenye vituo vya afya kupima, na kuanza matibabu ikiwa utagundulika na ugonjwa kwa kutumia dawa nyumbani au kwenda kituo cha afya kila siku.