RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, amezindua Jukwaa la Mfuko wa Kilimo Afrika (AGRF), huku akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuona Tanzania inakuwa ghala la chakula Barani Afrika ifikapo 2030. Aidha amesema matarajio yake ifikapo mwaka 2030 sekta ya kilimo utachangia Pato la taifa kwa asilimia 30 katika uchumi wa nchi.
Rais Samia ameyasema hayo jana, Ikulu Dar es Salaam wakati akizindua Jukwaa AGRF, pamoja na kutangaza mkutano utafanyijka Septemba 5-8 nchini.
Katika uzinduzi huo umesema Tanzania ina fursa ya ardhi yenye rutuba na vyanzo vya maji hivyo vikitumika ipasavyo, ni wazi sekta ya kilimo itachochea pato la taifa kukua kwa kasi.
Amesema kilimo kinachangia uchumi wa Tanzania kwa asilimia 25 ambacho ni muhimu katika kukuza maendeleo, hivyo jitihada zake ni kuona mchango huo unaongezeka kwa kasi kubwa.
Amesema katika kuonesha dhamira ya serikali kwenye kukuza kilimo Machi 20 mwaka huu atazindua mafunzo kwa vijana 812 mkoani Dodoma ambao wameomba kuwezeshwa kushiriki kilimo nchini. Amesema zaidi ya vijana 25,000 wameomba kujiunga na mradi wa kilimo kwa vijana na wanawake, hivyo anaomba wadau wengine kuja kuwekeza katika sekta hiyo kwa kushirikiana na makundi hayo.
Amesema jitihada za kuzalisha chakula safi na salama zinahitajika kwani nchi nyingi zinapitia wakati mgumu kutokana na ukame. “Nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia kwa miongo ya misinu minne hawana mvua za kutosha, hali ambayo imeongeza ukame, hivyo Tanzania tunawajibu wa kuzalisha kwa wingi ili tuweze kusaidia majirani zetu,” amesema hawatokuwa na mvua “Tunashukuru Mungu kwa kuwepo mvua na ardhi ya kutosha na fedha zipo za kukuza kilimo na kulisha katika Afrika, tunapaswa kuwekeza katika eneo hili,”amesisitiza.
Amesema mikakati yake ni kuona Tanzania inajitosheleza katika mazao ya chakula na biashara, na kuachana na uagizaji wa mazao kama ngano, sukari na mafuta.
Ametolea mfano kuhusu upungufu wa tani 30,000 za zao la sukari na kuwataka wazalishaji waongeze uzalishaji kuziba pendo hilo.
Dk. Samia amesema ili Tanzania iwe ghala ya chakula Afrika, ni muhimu kuongeza uzalishaji katika mazao yote ambayo ya ahitajika katika bara hilo. Amesema Serikali yake itahakikisha inatoa pembejeo, viuatilifu na mbolea kwa wakulima kote nchini. .
Amesema wamejipanga kupokea ushauri kutoka kwa Baraza la Kukuza Kilimo Tanzania alilolizindua jana, chini ya Mwenyekiti Mizengo Pinda,.
Pia amesema Serikali imeanzisha Mfuko wa Kuimarisha Kilimo ambao utaweza kusaidia wakulima nchini jambo ambalo litaongeza uzalishaji. .
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Unguja Kuna hoteli zaidi ya 600 ambapo bado hawajajitosheleza kwa bidhaa za kilimo na ufugaji, hivyo uzinduzi na mkutano wa kilimo utasaidia kukabiliana na hilo.
Amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliahidi kutoa ajira milioni 3 kwa Tanzania Bara na Zanzibar laki 300,000 hivyo ajira hizo nyingi zitatoka katika sekta hiyo , ambapo pia kuna vijana wengi wanamaliza vyuo vikuu na wapo waliokuwa hawajenda vyuo vikuu nao wataweza kufaidika huko.
Alieleza sekta ya kilimo inaendelea kuimarika, ambapo zao la mwani limekuwa linalimwa na wanawake hivyo mkutano huo utatoa fursa ya Kuja kuonyesha zao Hilo pamoja na uvuvi.
Awali Rais Mstaafu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chakula Afrika (URT), Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema zimetengwa Dola za Marekani laki 100,000 kwa ajili ya kuimarisha kilimo katika Afrika hususani kwa wanawake na vijana katika kuzallisha usalama wa chakula.
Naye Mwenyekiti wa AGRA, Waziri Mkuu mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn amesema Afrika inapaswa kujipanga kukabiliana na changamoto ya chakula kwa watu wake. Rais wa AGRA, Dk Agness Kalibata amesema taasisi hiyo itatumia mbinu mbalimbali kwa kushawishi wadau wa kilimo kusaidia sekta hiyo.