Na Mwandishi wetu
KATIBU Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amewataka wakazi wa vitongoji vya Losoito na Emishiye Kijiji cha Losoito Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kutunza mradi wao wa maji.
Chongolo akizungumza baada ya kutembelea mradi huo amewataka wakazi wa eneo hilo kutunza mradi huo kwani maji ni uhai.
“Tunawapongeza kwa kupata mradi huu wa maji ila mnapaswa kuutunza ili uwe endelelevu kwenu na mifugo yenu mnayopata huduma hii,” amesema Chongolo.
Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira viijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Joanes Martin amesema mradi huo umewezesha watu 2,204 wa vitongoji viwili vya Losoito na Emishiye kupata huduma ya maji.
Mhandisi Martin amesema mradi huo umekamilika kwa kutumia muda wa miezi mitano hivyo wakazi wa eneo hilo pamoja na mifugo yao wananufaika na maji hivi sasa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Losoito, Samson Swakei ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mradi huo wa maji.
Swakweli amesema kabla ya kupatikana kwa mradi huo walikuwa wanachangamoto kubwa kufuata huduma hiyo hadi mji mdogo wa Mirerani ambapo ni mbali na hapo.
Amesema walikuwa wanatumia punda kufuata maji umbali mrefu wa kilomita 30 kwenda na kurudi hivyo wameishukuru Serikali baada ya kupata huduma hiyo kwa karibu zaidi.