Waziri wa maji Jumaa Aweso (kulia) akiwa na Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam Karia wakisikiliza maelezo kutoka kwa maafisa wa maji katika ufunguzi wa kongamano la maji lenye lengo la kujadili changamoto zinazoikumba sekta hiyo ambalo linafanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam
……………..
NA MUSSA KHALID
Waziri wa maji Jumaa Aweso amekielekeza Chuo cha Maji kufuatilia pamoja na kufanya tathmini ya mienendo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji Nchini ili kuwa na majibu ya pamoja kwa maslahi mapana ya uchumi wa Taifa.
Waziri Aweso ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es salaam katika ufunguzi wa kongamano la maji lenye lengo la kujadili changamoto zinazoikumba sekta hiyo pamoja na kubadilishana uzoefu ambalo limedhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya –NMB.
Amesema ni wazi kuwa Chuo hicho ni kiuongo kikubwa katika kuzalisha wataalam watakaotekeleza miradi hiyo pamoja na kufanikisha Kilimo cha umwagiliaji kitakachomuinua mtanzania hasa wa hali ya chini.
Aidha Waziri Aweso amesema kufanyika kwa kongamano kwa mara ya pili ni moja ya njia ya kubadilishana uzoefu na mbinu kutoka nchi mbalimbali ili kuimarisha huduma ya maji hapa nchini.
‘Teknolojia na mazingira vinabadilika hivyo ni muhimu kubadilika na kwenda na wakati, na kusisitiza mabadiliko yanahitaji wataalamu zaidi katika kuendesha na kusimamia miradi ya maji’Amesema Waziri Aweso
Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Masoko wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini -RUWASA, Athuman Sharifu amesema kuanzia mwaka 2019 hadi 2022 upatikanaji wa maji Vijijini umeongezeka kwa asilimia 10 huku mkakati uliopo ni kufikia asilimia 85 ifikapo 2025.
Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam Karia amesema washiriki zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi wanashiriki kongamano hilo la kimataifa linalofanyika kwa mara ya pili hapa nchini.
Naye Meneja wa tawi la Benki ya -NMB Ubungo plaza, Sylvester Ngowi amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ili kufanikisha miradi mbalimbali ya huduma za maji kote Nchini.
Kongamano hilo ni la siku tatu ambalo limeanza March 8 na linatarajiwa kumalizika March 10 na kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya Maji.