Mhe. Slyvester Kainda, Msajili wa Mahakama ya
Rufani amefungua mafunzo ya wakufunzi kumi na sita (16) ambao ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhadhiri kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Makarani kumi nanne (14) kutoka Mahakama Kuu kanda za Mwanza, Arusha, Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam wanaotarajiwa kufundisha Watunza Kumbukumbu Wasaidizi (Makarani wa Mahakama) namna bora ya kushughulikia mashauri ya
mtoto.
Mafunzo haya yanayofanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo jijini Dar es Salaam yataendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa siku tatu kuanzia tarehe 08/03/2023 mpaka tarehe 10/03/2023 kupitia ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na haki za Mtoto (UNICEF).
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki tajwa mbinu
mbalimbali za kufundishia watunza kumbukumbu wasaidizi (Makarani wa Mahakama) namna bora ya kushughulikia mashauri ya watoto.
Ili kufikia malengo hayo mada zitazowezeshwa katika mafunzo hayo zinagusa eneo la majukumu na wajibu wa karani au msaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama katika kushughulikia mashauri ya mtoto kwa kuzingatia sheria ya mtoto ya mwaka 2009.
Wawezeshaji wa Mafunzo hayo ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.Nyigulila Mwaseba na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke Mhe. Aziza Mbadjo ambao ni wabobevu, wazoefu na mahiri katika eneo la haki mtoto.