………………..
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mtandao wa Polisi Wanawake (TPFNET) Mkoa wa Pwani ,umetoa msaada wa pazia maalumu la kumsitiri mgonjwa akihudumiwa (folding screen) katika zahanati ya Polisi ,Mkoa wa Pwani pamoja na cherehani kwa mama Getruda Elias Dastan, Mkazi wa Kilangalanga ,Wilaya ya kipolisi Mlandizi aliyetelekezwa na mume wake.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika katika Zahanati ya Polisi Wilaya ya Kibaha , katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Mwenyekiti wa mtandao huo Ariziki M. Makwaya- SSP ,alisema TPFNET kwa kuthamini huduma za kiafya zinazotolewa katika zahanati hiyo wameamua kununua pazia hilo maalumu ili kuboresha utendaji kazi wa zahanati.
“Alieleza,TPFNET wapo imara na wapo tayari kufanya kazi kama ambavyo kuna viongozi wengi wanawake katika Mkoa wa Pwani ambao ni yeye mwenyewe kama Mkuu wa Upelelezi Mkoa,Msaidizi wake,Mkuu wa Polisi wa Wilaya za Chalinze,Mlandizi na Kisarawe hivyo utendaji kazi wa askari wa kike utazidi kuimarika.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ambaye ndio mlezi wa TPFNET Pwani, Muhudhwari R. Msuya – ACP aliwapongeza kwa Jambo walilolifanya ni la kuheshimika na la busara kwa maslahi ya taifa.
Aliwasihi askari hao waendelee na moyo huo wa upendo na viongozi wapo tayari kuwatia moyo , kuwaunga mkono kuhakikisha kila jambo linafanikiwa.
Mkuu wa kikosi cha afya Mkoa wa Pwani, Peter Zablon – SP alisema tendo hilo ni la faraja kwake kama kiongozi na kikosi kwa ujumla na anaamini huo ni mwanzo
Kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ,Mkoa wa Pwani yanatarajiwa kufanyika tarehe 08 Machi 2023 katika Wilaya ya Bagamoyo.