Afisa Utawala kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Irene Kipwate (kulia) na Mwenyekiti wa wanawake wa wizara hiyo, Bi. Joyce Pallangyo ([katikati), wakikabidhi kwa niaba ya Watumishi wanawake wa Wizara hiyo msaada wa vifaa mbalimbali kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maalum Buigiri, Bw. Samuel Josan wakati walipowatembelea shule hiyo wilayani Chamwino mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Afisa Utawala kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Irene Kipwate akizungumza na uongozi na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maalum Buigiri wakati watumishi wa Wizara hiyo walipowatembelea shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani wilayani Chamwino, Dodoma.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maalum Buigiri, Bw. Samuel Josan, akitoa salamu za shukurani baada ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka kwa Watumishi wanawake wa Wizara ya Fedha na Mipango walipowatembelea shule hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Afisa Utawala kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Beatrice Masanja, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maalum Buigiri wakati Watumishi wanawake wa Wizara walipotembelea shule hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, wilayani Chamwino , Dodoma.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Maalum Buigiri, Bw. Godfrey Daudi, akitoa maelezo ya shule kwa Watumishi wanawake wa Wizara ya Fedha na Mipango walipotembelea shule hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, wilayani Chamwino, Dodoma.
Watumishi wanawake wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maalum Buigiri wakati walipowatembelea shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, wilayani Chamwino, Dodoma.
Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Maalum Buigiri wakifurahia jambo walipotembelewa na Watumishi wanawake wa Wizara ya Fedha na Mipango (hawapo pichani) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
………………………………..
Na. Saidina Msangi na Farida Ramadhani, WFM, Chamwino
Watumishi Wanawake Wizara ya Fedha na Mipango wametoa msaada wa mahitaji ya msingi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi na wasioona ili kuwawezesha kukidhi mahitaji yao.
Wametoa msaada huo walipotembelea Shule ya Msingi Buigiri iliyopo Wilaya ya Chamwino, yenye Watoto wenye mahitaji maalumu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 8.
Ziara hiyo iliongozwa na Afisa Utawala Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Irene Kipwate ambaye alieleza kuwa watumishi wanawake wa Wizara wameguswa na Watoto hao na kuona umuhimu wa kuwatembelea hasa katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ili kuzungumza nao na kuwapatia msaada huo.
‘’Tumekuja kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, kuwaona na kuwapatia zawadi tulizokuja nazo, kama mama tumefarijika kuwatembelea watoto hawa ambao kwa umri huu mdogo walipaswa kuwa na wazazi wao lakini kutokana na changamoto za kiafya wako hapa hivyo tunawapongeza walimu na walezi kwa kazi nzuri mnayoifanya kwani Watoto wana afya njema’’, alisema Bi. Kipwate.
Alisema kama wazazi wanatamani kuona Watoto hao wakifikia ndoto zao hivyo kwa nafasi yao wataendelea kuwatembelea na kutoa misaada kwa kadiri watakavyoweza.
Aidha, alitoa wito kwa wanawake na wananchi kwa ujumla wajitoe kusaidia Watoto hao kwani wana mahitaji mengi hivyo wakumbuke kituo hicho licha ya Serikali na Kanisa kuhudumia kituo hicho na vingine, wananchi waguswe kuwaona Watoto hao na kuwapatia misaada mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya wanawake Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Joyce Pallangyo, ameshukuru uongozi wa shule hiyo kwa kuwapokea na kuwashukuru waalimu na walezi wa shule hiyo kwa huduma wanayotoa kwa Watoto hao na kuwaombea baraka kwa kazi hiyo njema.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hiyo Mwl. Samwel Sospeter Jonathan, ameshukuru uongozi wa Wizara kwa kuwatembelea Watoto wenye mahitaji maalumu na kuwapatia msaada ambao utawasaidia Watoto kukidhi mahitaji yao muhimu.
‘’Ugeni huu tumeupokea kwa furaha kubwa kwani umesaidia upatikanaji wa mahitaji ya msingi ya kila siku kwa Watoto hawa ambao wanatoka katika familia duni, tunatoa wito kwa jamii ya Watanzania kuyatambua makundi haya na kuyapa kipaumbele pamoja na kuyatembelea’’ alisema Mwl. Jonathan.
Alitoa rai kwa wadau mbalimbali nchini kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa matibabu kwa Watoto hao kwani shule haina fungu la matibabu hivyo inapata changamoto kuwapatia Watoto huduma za afya pindi wanapougua.
Pia ametoa wito kwa watumishi wa Wizara hiyo kuwa mabalozi wao kwani shule hiyo sio ya kibiashara kwa wadau kusaidia shule hiyo kujenga uzio ili kuimarisha ulinzi na usalama wa Watoto wenye ulemavu wa Ngozi wanaosoma shuleni hapo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo Monica Isaya anayesokma darasa la saba katika shule hiyo aliwashukuru watumishi wanawake wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwatembelea na kuwapatia msaada wamefarijika na kuahidi kujitahidi katika masomo yao licha ya ulemavu walionao watafanya vizuri katika masomo yao.
Watumishi hao wamekabidhi vitu mbalimbali ikiwemo taulo za kike, mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia, vyakula pamoja na vifaa vya usafi na kuahidi kuwatembelea wakati mwingine.
Shule ya Msingi Buigiri ni ya pekee mkoani Dodoma, ilianzishwa Aprili 30, 1950 kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 120 inafundisha Watoto wenye uoni hafifu, wasioona pamoja na wenye ulemavu wa ngozi kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba ambapo kwa miaka kumi mfululizo imeshika nafasi ya kwanza Kiwilaya katika matokeo ya darasa la nne na la saba.