Na Dotto Mwaibale, Singida
KIWANDA cha kukamua mafuta ya kula ya alizeti cha Singida Fresh Oil Mill,
kimemuomba Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo,kusaidia
kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazozoletesha uzalishaji ikiwamo kuwepo kwa
vizuizi vingi katika usafirishaji wa bidhaa za mazao ya kilimo vinavyowekwa na
halmashauri.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Khalid Ally Omary almaarufu Shulu ametoa ombi
hilo Leo Machi 4, 2023 baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Chongolo alipotembelea
kiwanda hicho kuangalia uzalishaji ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake mkoani
hapa.
Omary alimweeza Katibu Mkuu wa CCM kuwa changamoto ambazo zimekuwa kero katika
uendeshaji wa kazi ni kuwepo kwa vizuizi vingi wakati wa usafirishaji wa bidhaa
za mazao ya kilimo katika barabara kuu.
“Ukisafirisha mashudu ya
alizeti kutoka Singida kwenda Kenya utapitia Singida,Oldonyosambu na Longido
unatozwa ushuru kila eneo kwa bidhaa hiyo wakati jirani zetu Uganda hawana tozo
yeyote ya bidhaa hiyo wakipeleka Kenya, hali hii inasababisha ugumu kushindana
na waganda ambao tunategemea soko moja Kenya,” alisema Omary.
Ally alitaja changamoto nyingine kuwa ni kukatikatika kwa umeme kila mara
na kusababisha uharibigu wa mashine, ubovu wa barabara na uhaba wa alizeti ya
kutosha.
Mkurugenzi huyo alisema kwa Sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kukamua Tani
90 kwa siku za alizeti na kupata lita 23,300 za alizeti lakini kutokana na
ukosefu wa alizeti ya kutosha kinakamua tani 22 tu na kupata mafuta kita 6,600
kwa siku.
Naye Chongolo akizungumza baada ya kukitembelea kiwanda hicho Chongolo
alisema halmashauri ziache tabia ya kuvizia
kila kinachopita kwao wakichukue kwani jambo hilo linaweza kusababisha maeneo
mengine yashindwe kupelekewa bidhaa.
“Hebu fikiria mtu atoke na samaki wake mjini Mwanza afike Misungwi
achajiwe,apite Kishapu achajiwe,aje Shinyanga achajiwe,aje Nzega achajiwe,aje
Igunga achajiwe,apite Iramba,Mkalama na Singida achajiwe,afike Ikungi hadi
Manyoni achajiwe, Sasa je bidhaa hiyo hadi ifikishwe Dar es Salaam itauzwa kwa
shilingi ngapi,” alisema.
Chongolo alisema hali hiyo inakuwa hivyo kwasababu kila halmashauri
inashindwa kubuni mfumo na uwekezaji wa kwao na hivyo kutaka kuibukia na
kutengeneza sheria ndogo zenye lengo la kuwaumiza wengine jambo ambalo CCM
haikubariani nalo.
Alisema ni lazima mamlaka zinazohusika ziweke mifumo na sheria ndogo ambazo
zitakwenda kusimamia ukusanyaji wa mapato katika halmashauri na kwamba sheria
hiyo ziwekwe wazi kwenye mazao yanayozalishwa katika eneo husika ili kudhibiti
kudai ushuru katika kila eneo mazao yanapopita.
Chongolo kabla ya
kutembelea kiwada hicho alifungua mradi
wa kiuchumi wa fremu za maduka katika eneo la Ofisi za CCM mkoa Singida mjinina
vile vilivyopo Uwanja wa Namfua.