Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo alipozungumza na wakazi na wanachama wa CCM Shina namba 5, Tawi la Iguguno Kaskazini, kata ya Iguguno wilaya ya Mkalama.
Katibu Mkuu yupo kwenye ziara mkoani Singida yenye lengo la kukagua, kuhamasisha, kuhimiza na kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Na Dotto Mwaibale, Mkalama
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida James Mkwega amemuomba Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo kuongeza idadi ya walimu ambao hawatoshi wilayani huko.
Mkwega alitoa ombi hilo kwa Chongolo wakati wa siku ya nne ya ziara yake ya kukagua ilani ya chama hicho na kukagua miradi ya maendeleo wakati akizungumza na wananchi wa shina namba tano Kata ya Iguguno.
“Ndugu Katibu Mkuu Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutoa fedha na kujenga madarasa katika halmashauri yetu lakini changamoto kubwa iliyopo hatuna walimu wa kutosha tunaomba ukatuombee hatusaidie katika hilo” alisema Mkwega.
Chongolo akielezea changamoto hiyo alimuhakikishia Mkwega kuwa jambo hilo atalifanyia kazi na kuangalia usawa wa walimu kati ya wa mjini na vijijini.
Wakati huohuo Chongolo amesema atakwenda kuwaona wahusika na kuwahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kujengwa kwa barabara ya kiwango cha lami kutoka Iguguno, makao makuu ya wilaya ya Mkalama Nduguti.
Aidha Chongolo alisema barabara hiyo haitaishia Nduguti pekee bali atafika hadi Sibiti wilayani Meatu na kuunganisha mikoa ya Manyara na Arusha.
Chongolo alitoa maelezo hayo kufuatia ombi lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Francis Isack kuomba kujengwa kwa barabara hiyo ya kilometa 42.