Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Esther Mkokota akizungumza leo tarehe 1/3/2023 jijini Dar es Salaam wakati akitoa elimu kwa viongozi wa Manispaa ya Temeke wakiwemo madiwani, maafisa watendaji kata kuhusu programu ya ‘TAKUKURU –Rafiki’.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Mhe. Abdallah Mtinika akizungumza leo tarehe 1/3/2023 jijini Dar es Salaam na viongozi wa Manispaa ya Temeke wakiwemo madiwani, maafisa watendaji kata kuhusu programu ya ‘TAKUKURU –Rafiki’.
Baadhi ya madiwani, maafisa watendaji kata Manispaa ya Temeke wakipewa elimu kuhusu programu ya ‘TAKUKURU –Rafiki’.
…………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Madiwani wa Manispaa ya Temeke wametakiwa kutumia programu ya ‘TAKUKURU Rafiki’ ili kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza leo tarehe 1/3/2023 jijini Dar es Salaam wakati akitoa elimu kwa viongozi wa Manispaa ya Temeke madiwani, maafisa watendaji kata kuhusu programu ya ‘TAKUKURU -Rafiki” Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Esther Mkokota, amesema kuwa programu hiyo ina lengo la kuwa karibu na wananchi katika kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya rushwa.
“TAKUKURU – Rafiki inatekelezwa kupitia vikao katika ngazi ya kata, tunapata fursa ya kutambua kero zilizopo kwenye utoaji au upokeaji wa huduma kama za afya au elimu pamoja na mchakato wa kutekeleza miradi ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu ya maji” amesema Bi. Mkokota.
Bi. Mkokota amesema kuwa kero za wananchi zikiachwa pasipo kutatuliwa au kupatiwa ufumbuzi zinaweza kusababisha kutokea kwa vitendo vya rushwa katika jamii na kuleta usumbufu mkubwa.
Amesema kuwa katika vikao ngazi ya kata viongozi wa kisiasa, watendaji wa serikali, wazabuni pamoja na wananchi wanapata fursa ya kushirikiana katika kutatua kero au kuweka mikakati ya jinsi kuzitatua kwa pamoja.
Amebainisha kuwa programu ya ‘TAKUKURU – Rafiki’ inachangia kukuza ustawi wa utawala bora kwa kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa umma au katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Programu hii itasaidia kuongeza uzingatiaji wa misingi ya utawala bora, ushirikiano wa kila mwananchi na wadau katika kupambana dhidi ya rushwa na kuaminika kwa serikali kwa jamii inaowahudumia” amesema Bi. Bi. Mkokota.
Ametoa wito kwa wananchi na wadau wengine kutumia lugha rafiki katika kushirikiana kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia ‘TAKUKURU – Rafiki’.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Mhe. Abdallah Mtinika amewataka madiwani wa Mamispaa ya Temeke kupitia vikao vyao na wananchi wawe na utamaduni wa kuwaalika TAKUKURU ili kusikiliza kero pamoja na kutoa elimu kuhusu vitendo vya rushwa.
Hata hivyo madiwani pamoja na maafisa watendaji kata kutoka kata mbalimbali Manispaa ya Temeke wamefurai baada ya kupata elimu kuhusu TAKUKURU Rafiki, huku wakibainisha kuwa wataendelea kuitumia TAKUKURU katika kuhakikisha jamii inaelimika.
‘TAKUKURU – Rafiki’ ni programu iliyoanzishwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuongeza ushiriki wa kila mwananchi pamoja na wadau mbalimbali.