Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MWENYEKITI wa kamati ya usalama mkoa wa Pwani ,alhaj Abubakari Kunenge, ameviagiza vyombo vya usalama pamoja na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuwakamata na kuwachunguza vinara zaidi ya 100 waliojihusisha na kuchochea wavamizi na uuzaji maeneo Kata ya Mapinga.
Ameeleza ,watu hao ni watuhumiwa kuanzia Sasa ,wahojiwe na kufanyiwa uchunguzi kwani ndio chanzo cha kukithiri kwa migogoro ya ardhi Mapinga, na kusababisha kuifikisha Kuwa kata kinara nchini kwa kuongoza kwenye migogoro ya ardhi.
Akitoa Maamuzi ya kamati ya utatuzi wa migogoro ya Waziri wa Ardhi Angelina Mabula ,Mtambani Kunenge alieleza ,atafanya mazungumzo na IGP pamoja na Mkurugenzi wa TAKUKURU kuongeza nguvu ya kutosha ili kuisafisha kata hiyo bila kumuonea mtu ,na haki itatendeka.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya usalama mkoa ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Pwani,alieleza taarifa za watu hao vinara(watuhumiwa majina yamehifadhiwa) , wameipata kupitia taarifa siri (kiitelijensia) na wakati wa uchambuzi wa kesi za migogoro ya ardhi kwenye Maeneo mbalimbali kwenye kata hiyo.
Alieleza ,katika orodha hiyo yapo majina vinara wa kuchochea wavamizi, baadhi ya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi waliojihusisha kuuza maeneo na majina ya ziada wakiongozwa na aliyekuwa diwani wa kata hiyo Ibrahim Mbonde.
Alieleza,kamati imeridhia na Wizara na kuamua watu wawekwe hadharani na kukamatwa ,wahojiwe na kuchunguzwa na endapo wakithibitika na tuhuma hizo na kukutwa na jinai sheria ichukue mkondo wake.
“Sheria ni msumeno ,hakuna atakaeachiwa kwa hili kama atabainika kuhusika,kama wapo watumishi wapewe tuhuma zao wakigundulika Mkurugenzi wa Halmashauri pia uwasimamishe kazi ili hatua stahiki zifuate”
Kunenge alibainisha kwamba ,wale wa Chama Cha Mapinduzi kama wamebainika ni kwamba watakuwa wameenda kinyume na Chama ,Chama itabidi kiwaweke pembeni kwa taratibu za kichama”
Alikemea maeneo yenye migogoro yasiuzwe na yasiendelezwe kamati ya usalama isimamie hadi ufumbuzi utakapopatikana.
Aliwaomba wananchi watoe ushirikiano mahakamani endapo watahitajika katika ushahidi na wasiogope kujiweka pembeni.
“Ole wake atakaebainika kuwasumbua wananchi kwasababu wametoa taarifa,nimesikia hapa Kuna kundi linajiita Mung’iki Kuwa wameiweka Serikali Mkononi ,siatawavumilia “
Alivitaka vyombo vya usalama kutumia nguvu itakayohitajika kwa wale watakaowadhuru Askari polisi au wananchi,kwani Serikali ya mkoa imedhamiria kupambana na matukio ya migogoro ya ardhi Mapinga.