……………………….
Ikiwa zimepita siku takribani 14 Tangu kuulizwa swali kwa Naibu Waziri mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini kuhusu ujenzi wa Kituo cha Polisi Mchinga na uchakavu wa Gereza la Kingurungundwa swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Mchinga Salma Kikwete, Naibu Waziri Mmambo ya Ndani ya Nchi ametembelea maeneo hayo na kujionea hali halisi ilivyo.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo Sagini ameelekeza kutengwa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Polisi Mchinga ili kunusuru hali ya kituo hicho kwa sasa wakati maandalizi ya ujenzi wa Kituo kipya na cha kisasa katika eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya ujenzi ukianza.
“Kwa viwango vyovyote jengo hili halifai kuwa Kituo cha Polisi. Mazingira ya Kituo hata wahalifu sugu hawawezi kukaa humu na zaidi usalama wa Askari wetu ni hatarishi. Mnastahili kuwa na Kituo chenye hadhi ya Tarafa. Hiki kikarabatiwe kwa haraka ili kiendelee kutumika wakati tunaanza ujenzi wa kituo kipya katika eneo stahili kwani hata eneo kilipo kituo cha sasa ni karibu na barabara na ni hatarishi.”Alisema Sagini
Kuhusu ujenzi wa majengo ya Gereza la Kingurungundwa Sagini amesema kuwa Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa maeneo ya Magereza kote Nchini na amesema kuwa vipaumbelea vimeendelea kutolewa katika maeneo yenye mazingira chakavu na atahakikisha pia Gereza la Kingurungundwa linaingizwa kwenye mpango kutokana na uchakavu wake.
Mbunge wa Jimbo la Mchinga Salma Kikwete amesema kuwa miongoni mwa changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa katika Jimbo la Mchinga ni pamoja na ukosefu wa Kituo bora cha Polisi na uchakavu wa majengo katika gereza la Kingurungundwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya hali ya Kituo hicho kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi ACP Mtaki Kurijila amesema kuwa kituo hicho ambacho kilijengwa takribani miaka 20 iliyopita kwa nguvu za Wananchi hakikuzingatia michoro ya ujenzi wa vituo vya Polisi na kimekuwa na manufaa na muhimu kwani kinahudumia Vijiji 39 vilivyopo katika Jimbo la Mchinga licha ya uchakavu wa miundombinu iliyopo.
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wa Jimbo la Mchinga akiwemo Juma Mshirazi na Aziza Ngumbe wamesema kuwa wanashukuru kwa ziara ya Naibu Waziri kufika katika Kituo hicho na kujionea hali halisi na wameomba ujenzi wa Kituo kipya kuharakishwa ili kuondoa changamoto kwa askari na pia watuhumiwa ambao wanaweza kutumia mianya ya ubovu wa miundombinu kutoroka.