Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Jaffar Haniu ametembelea vyombo vya habari vilivyopo Wilayani Rungwe na kujionea vipindi mbalimbali vinavyorushwa vituo hivyo sambamba na kuzungumza na wananchi.
Vituo alivyotembelea ni pamoja na redio Rungwe na Chai FM vyote vikiwa Tukuyu Mjini.
Katika vituo hivyo kwa nyakati tofauti Mhe. Haniu ameeleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali hivyo vyombo hivyo havina budi kuandaa vipindi vitakavyoelimisha jamii, kuhamasisha, kuikosoa na kuburudisha jamii.
Mhe.Haniu ambaye kitaluma ni Mwanahabari, ameeleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule kufanya hivyo mapema ili kuwawezesha kupata haki yao ya Msingi kwa Maendeleo na Ustawi wa taifa la Tanzania.
Ameeleza kuwa Tanzania kupitia Mradi wa Boost imeanza kuboresha miundombinu ya kutolea huduma ya elimu ya Msingi ambapo Ujuzi kwa walimu, Vitabu, Vyoo na madarasa yatajengwa.
Akizungumzia Sekta ya Kilimo, Mhe Haniu amesisitiza kuwa Serikali imeendelea kusambaza Mbolea ya Ruzuku kwa Wakulima Wilayani Rungwe na kuonya Mawakala pamoja na wakulima wanaouza na kununua Mbolea hiyo kwa njia ya udanganyifu kuacha kufanya hivyo kwani wanarudisha nyuma juhudi za Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kuwaletea Maendeleo wananchi Wake.
Aidha Mhe. Haniu ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha masoko ya bidhaa mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo ( Wamachinga) ili kutoa fursa ya kujiongezea kipato Cha kila siku.
” Ndugu zangu wananchi niwambie, unapojengewa soko maana yake kumsaidia mteja ajue bidhaa ipi ataipata wapi. Vivyo hivyo wamachinga, soko la ndizi na bidhaa zingine Masoko haya yamesaidia sana likiwemo soko la Mwambenja lililofunguliwa Leo”
Mhe. Haniu ameagiza wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyotengwa kwa nia nzuri ya kuboresha mandhari ya mji, Usafi wa mazingira, Mapato ya Serikali na Usalama wa Mali zao.
Katika hatua nyingine Mhe Haniu ameagiza wakazi wa Wilaya ya Rungwe kuacha migogoro ya ardhi na kuwa imekuwa ikihatarisha amani na utulivu katika Jamii.
Amesema Ofisi yake pamoja na Mabaraza ya ardhi amekuwa akitatua migogoro mbalimbali ya ardhi sambamba na utoaji elimu dhidi ya Matumizi bora ya ardhi na kuandika Wosia kwa ngazi ya kaya hali itakayomaliza migogoro hiyo katika Wilaya ya Rungwe.