Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo akisisitiza jambo wakati wa kikao.
Meneja wa Shoroba kutoka katika Shririka lisilo la kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP), Joseph Mwalugelo akiongea na waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) waliofanya ziara ya siku nne wilayani Kilombero.
Joseph Mwalugelo (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
Njia ya chini ya barabara ambayo ni maalumu kwa kuwawezesha tembo kupita bila kuleta madhara katika jamii.
………………………………
Na Sidi Mgumia, Morogoro
Miundombinu ni muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote ambalo linahitaji kusonga mbele kiuchumi, kijamii, kwasababu husaidia wananchi na Serikali katika kufanikisha malengo iliyojiwekea katika kutunza wanyamapori na mazingira kwa ujumla.
Kukosekana kwa miundombinu ya uhakika kunachangia Tembo kuharibu mazinigira lakini pia kuchochea migogoro kati ya wanyamapori na binadamu waishio kando ya hifadhi za taifa.
Kwa muktadha huo, suluhu ya kudumu yakutatua migogoro hiyo inatajwa kuwa ni ujenzi wa uzio wa kisasa wa umeme kwenye shoroba haswa ile inayoounganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Udzungwa kupitia msitu wa asili wa Magombera, Kijiji cha Kanyenja, Sole na Mangula A.
Hayo yanabainishwa na Joseph Mwalugelo, Meneja wa Shoroba kutoka katika Shririka lisilo la kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) waliofanya ziara ya siku nne wilayani Kilombero.
Waandishi hao wa mazingira wanatekeleza mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kutembelea na kuangazia changamoto zinazozikabili shoroba mbalimbali nchini Tanzania.
Mwalugelo alisema kuweka uzio wa umeme ndio itakuwa suluhu ya kudumu katika kutatua migogoro kati ya Tembo na binadamu lakini pia kutunza mazingira na kuwalinda Tembo na jamii kwa ujumla.
“Tumekuwa tukijaribu njia tofauti za kuzuia Tembo kufanya uharibifu katika mashamba ya wanakijiji zikiwemo za uzio wa harufu, mabati, taa za sola na mizinga ya nyuki lakini bado hazikumaliza tatizo, hivyo tukaamua sasa kuanza mchakato wa kuweka uzio wa umeme kwenye shoroba hii ya Kilombero ambayo tunaamini ndio itakuwa suluhu ya kudumu,” alisema Mwalugelo
Aliongeza kuwa kupitia mradi wa Shoroba ya Tembo Kilombero ambao unatekelezwa na STEP katika vijiji vya Mang’ula A, Sole na Kanyenja wanamatarajio makubwa kuwa watafikia malengo kwakua tafiti nyingi zimeonyesha kuwa uzio wa umeme katika shoroba umeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa wakiangazia nchi jirani kama Kenya na namna ilivyoleta mafanikio.
Sambamba na hilo, ameongeza kuwa njia nyingine za kuzuia changamoto ya wanyamapori ni pamoja na njia na madaraja ya chini ya reli na barabara ambazo ni maalumu kwa kuwawezesha Tembo kupita bila kuleta madhara katika jamii.
Akizungumzia ujenzi wa njia hizo za chini anasisitiza kuwa zitazuia Tembo kuingia kwenye mashamba ya watu na kufanya uharibu.
“Kiukweli Tembo wanapokuwa wanatembea kwa kiasi kikubwa wanasababisha madhara mengi katika jamii, watu wanauwawa, wanaumia, nyumba zinabomolewa na mashamba kuaharibiwa. Hatua ya Tembo kupita katika njia zao rasmi itahakikishia usalama wa chakula wanakijiji lakini pia kupunguza usumbufu kwa wanafunzi Tembo wanapovamia maeneo ya shule mahali ambapo inasemekana kulikuwa ni njia za Tembo kwa muda mrefu, alisema Mwalugelo
Mwalugelo aliongeza kuwa matukio yapo na takwimu za kuuwawa kwa bindamu zinaonyesha mwaka 2018 mtu mmoja aliuwawa na Tembo, 2019 pia aliuwawa mtu mmoja, 2020 mmoja, 2021 walifariki watu wawili na 2022 waliuawa wengine wawili.
Lakini pia Tembo nao wamekuwa wakigongwa na treni ambapo kwa mwaka 2021 waligongwa tembo wawili na 2022 waligongwa wanne, matukio haya yametokea katika vijiji vya Kanyenja, Sole na Mang’ula A.
Kwakua mradi ulikuwa mpya kwa wanakijiji, STEP ilifanya jitihada kubwa ya kutoa elimu mara kwa mara kwa jamii juu ya umuhimu wa uwepo wa shoroba ya kisasa, kutunza mazingira, kuokoa Tembo na kuwaeleza wanakijiji kuwa wanamaanisha nini kwa kuleta huo mradi na namna watakavyonufaika nao.
Baada ya wanakijiji kuuelewa na kuupokea mradi kupitia elimu iliyotolewa, waliamua kwa hiari yao kuyatoa mashamba yao maeneo ya bonde la Kilombero ambayo yako katika maeneo ya shoroba ili kupisha shughuli za mradi ziendelee.
Katika harakati za kueleimisha jamii pia hawakuwaacha watoto nyuma kwani waliwaelimisha ili kuwatoa woga juu ya Tembo na kwamba sio adui bali anafaa pia kulindwa.
Vilevile, migogoro hiyo ikiwa ni changamoto ya Taifa kwa ujumla, viongozi wa mkoa nao wanawaunga mkono wadau hao wa mazingira katika juhudi za kutatua ama kuimaliza kabisa migogoro kati ya wanyamapori na binadaamu.
STEP kwa msaada wa Serikali na mashirika ya World Land Trust, Quick Respond na wengineo waliweza kusaidia zoezi la fidia ambalo lilitekelezwa baada ya tathimini zilizofanywa kwenye maeneo husika pia kwa kufuata taratibu za mpango wa matumizi ya ardhi na kushirikisha kikamilifu Uongozi wa Sereikali za Vijiji kama sheria inavyotaka.
Hata hivyo, kabla ya miezi sita kutimia kama sheria inavyosema, timu yao iliweza kukusanya pesa za kutosha na kuwalipa wanakijiji wa Sole, Kanyenja na Mangula A mwaka 2022 kwa tathimini iliyofanywa mwaka 2021.
Mwalugelo alisema kuwa tathimini zilifanyika kulingana na kilichopo shambani lakini pia ukubwa wa eneo la mtu.
Kulikuwa na mashamba ya mazao ya mpunga na miwa lakini pia kulikuwa na maeneo ambayo hayajaendelezwa, hivyo fidia ilitofautiana.
Fidia ya mashamba 179 yaliyofanyiwa tathimini kwa vijiji vyote vya Sole, Mangula A na Kanyenja ilikuwa takriban shilingi za kitanzania bilioni 1.7.
Pamoja na hilo, tathimini ya pili kwa wale ambao hawakuwepo wakati wa zoezi la kwanza kwasababu mbalimbali, imefanyika na wahusika watalipwa hivi karibuni, wao wanatarajiwa kulipwa kwa ujumla kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 261, kwa watanzania takriban 52.
Mohamed Libongoi ni mnufaika wa fidia kutoka kitongoji cha Mikoroshini anaeleza kuwa wanashukuru wamelipwa fidia ya mashamba yao na kuhusu mradi wa kurudisha na kutengeneza shoroba, anasema wameupokea na wanaamini utakwenda kumaliza changamamoto wanazaopitia.
“Huu mradi umepokelewa kwa asilimia 75 japo wapo walioukataa. Jitihada za Serikali za nini kinafanyika tunazielewa. Imani yetu ni kwamba mpaka mradi unakuja katika maeneo yetu ni lazima utafiti umeshafanyika kwa hivyo ni vyema sisi tukawaunga mkono katika jitihada hiyo, kwani inawezekana kitakachofanyika kitaweza kuondoa hii adha ya tembo kwetu, alisema Libongoi
Libongoi anasema yeye binafsi mwaka 2020 alipata hasara kwani Tembo walimharibia shamba lake lote la mpunga lenye ukubwa wa heka moja na robo tatu.
Kwa upande wake mnufaika Mrashi Dongwe wa kijiji cha Sonjo, Kata ya Mkula anayejishughulika na kilimo cha miwa, anasema shamba lake lipo eneo la Mangula A mahali ambapo pamejengwa daraja ambalo litasaidia Tembo kupita chini yake.
Elimu ya kutosha ya mradi wa shoroba kutoka STEP ndiyo iliniaminisha kuwa mradi ni wa kweli na kama wanakijiji tukakubali na Serikali ikaja ikafanya tathimini na kwa kila mkulima tukalipwa kulingana na ukubwa wa maeneo yetu, alisema Dongwe
“Nimelipwa zaidi ya shilingi milioni 24 kwa shamba lenye ukubwa wa heka mbili na robo tatu, pesa ambazo baada yakuzipata kama mwanamke zimenisaidia kufanya mambo yangu ya msingi katika familia pia niliongeza shamba jingine hivyo sikupata hasara,”alisema Dongwe
Kutokana na umuhimu wa mradi, Dongwe ameiomba Serikali isaidie kutekeleza mradii huo kwa haraka ili Tembo waweze kuongoza kwenye hiyo shoroba kwasababu mpaka sasa bado wanendelea kupita kwenye maeneo yao na kuwaharibia mazao mengine wanayoyategemea kuwasaidia na familia zao.
Kwa upande wa Serikali, Wendo Isidory ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Sole, Kijiji chenye watu 1010 wanaojishughulisha na kilimo, ambao kati yao wanawake ni 567 na wanaume 463, anasema mradi umeanza vizuri na watu wengi wameshalipwa fidia. Ingawa kuna wachache hawajalipwa, lakini wanaamini mradi huu utakapokuja kukamilika utasaidia kupunguza changamoto nyingi sana hasa za Tembo.
Tunaamini changamoto hii itatatuliwa kwa kiasi kikubwa ili kunusuru uchumi kushuka, tumekuwa tukisumbuliwa na Tembo ambao wamekuwa wakiharibu mashamba na kula matikiti, miwa na mpunga lakini kusumbua hata watoto shuleni wakati wa masomo, alisisitiza Isidory