Baadhi ya magari yanayomilikiwa na vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) wilayani Tunduru yakiwa yamepaki kwenye viwanja vya Chama Kikuu cha Ushirika(TAMCU LTD)baada ya kumalizika kwa minada ya zao la korosho.
****************************
Na Muhidin Amri, Tunduru
UZALISHAJI wa zao la korosho mkoani Ruvuma,umeshuka kutoka kilo milioni 25 msimu wa kilimo 2021/2022 hadi kufika kilo milioni 15.264 katika msimu 2022/2023,huku sababu kubwa ikitajwa wakulima kutokuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya viuatilifu na maafisa ugani kutowafikia wakulima kwa wakati.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu Ltd)Mussa Manjaule,amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa kikao cha wajumbe wa bodi ya Chama hicho kilichofanyika katika ofisi za Tamcu mjini Tunduru.
Manjaule amesema,Tamcu imepanga kuajiri maafisa ugani waliosomea zao hilo ambao watakwenda kuinua uzalishaji kwa kutoa elimu ya kilimo bora cha korosho,uzalishaji wa miche bora na matumizi ya pembejeo kwa wakulima kama mkakati wake wa kuongeza uzalishaji katika msimu 2023/2024.
Amesema,suala la kuajiri maafisa ugani na kuwapeleka katika maeneo yote yanayolima zao la korosho limepewa umuhimu mkubwa hasa baada ya kubaini baadhi ya maafisa ugani hawana uelewa mkubwa na hawajikiti sana kwenye zao hilo.
Manjaule ambaye ni mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa bodi ya Korosho Tanzania amesema,tatizo hilo limesababisha wakulima wengi kuendelea na kilimo cha mazoea na hivyo kushindwa kuleta tija inayokusudiwa.
“tumebaini moja ya sababu ya kushuka kwa uzalishaji wa korosho katika msimu 2022/2023 ni wakulima wetu kutofikiwa na elimu ya matumizi ya viuatilifu na kukosekana kwa maafisa ugani waliosomea zao la korosho,tumejipanga kuajiri maafisa ugani ambao watakwenda kuinua kiwango cha uzalishaji na ubora wa zao hilo ”amesema Manjaule.
Aidha,ameishukuru serikali kupitia wizara ya kilimo,kwa kupeleka pembejeo kwa wakati na kuwaasa maafisa ugani waliopo kuwa na utaratibu wa kuwatembelea wakulima na kuwapa elimu ya kilimo bora itakayowezesha kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Kwa upande wake Afisa ushirika wa wilaya ya Tunduru George Bisani, amewaasa wakulima kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo kwa kufanya palizi hasa kipindi hiki cha masika ili kuruhusu miti ya korosho kunyonya maji.
Amewashauri kulima mazao mengine ya biashara kama ufuta,soya,mbaazi ili kujiongezea kipato badala ya kuendelea kutegemea zao moja tu la korosho na Chama Kikuu cha Ushirika kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kiweze kujitegemea na kujiendesha.
Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika Tamcu Ltd Iman Kalembo amesema,katika msimu wa mwaka 2022/2023 chama hicho kimekusanya na kuuza korosho tani 15,264 kutoka kwa wakulima ambazo zimewaingizia jumla ya shilingi bilioni 26,724,000.
Amesema, wakulima wote wa zao hilo wanaosimamiwa na Tamcu kutoka wilaya ya Tunduru,Mbinga,Nyasa,Songea Namtumbo,Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma na Kyela mkoa jirani wa Mbeya wamelipwa fedha zao.
Amewashukuru viongozi wa serikali ya wilaya ya Tunduru wakiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro ,kwa kuwapa ushirikiano mkubwa uliowezesha minada 11 ya korosho kufanyika kwa amani na utulivu.
Amewaomba wakulima ambao ni wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos),kuvitumia vyama na viongozi wao katika uzalishaji wa zao hilo linalotajwa kuwa miongoni mwa mazao yenye mchango mkubwa wa uchumi wa nchi yetu.
Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika( Kidompu Amcos)Seif Mtamila,ameiomba serikali kupitia Halmashauri za wilaya kuwasimamia mawakala wa pembejeo na makampuni ili waweze kusambaza viuatilifu kwa wakulima ili kuwahi msimu wa kilimo.
Amesema,moja kati ya changamoto iliyochangia kushuka kwa uzalishaji wa korosho katika msimu 2022/2023,baadhi ya wakulima walichelewa kupata pembejeo kwa muda sahihi.
MWISHO.