Chifu wa Tano wa Kabila la wangoni Nkosi Emanuel Zulu Gama ambaye alisimikwa kuwa Chifu wa Wangoni mwaka 2001 ambaye anaendelea kuwa Chifu wa wangoni hadi sasa
Kaburi la Mviringo la Chifu wa wangoni Nkosi Mharule Zulu Gama ambaye alitokea Afrika ya Kusini na kufika kijiji cha Mbingamharule wilayani Songea mkoani Ruvuma,alikuwa chifu wa kabila la wangoni kuanzia mwaka 1847 hadi 1889 alipofariki na kuzikwa kwa mila na desturi za kichifu ambapo alizikwa na watu wawili wakiwa hai katika kijiji cha Mbingamharule.
Mzee Ngonyani mwenye umri wa miaka 90 ambaye ni Mzee wa Mila na Desturi katika kijiji cha Mbingamharule wilayani Songea mkoani Ruvuma
……………….
MOJA ya vivutio vya utalii wa kiutamaduni vinavyopatikana katika kijiji cha Mbingamharule wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ni uwepo wa kaburi la duara ambalo Chifu Nkosi Mharule bin Zulu Gama alizikwa mwaka 1889.
Mambo ambayo yanawashangaza wengi wanaotembelea kaburi hili ni historia inayoonesha kuwa Nkosi Mharule baada ya kufariki alizikwa kwa desturi na mila za kichifu za kabila la wangoni toka Afrika ya kusini.
Christian Ngonyani mwenye umri wa miaka 87 ni mzee wa Mila katika kijiji cha Mbingamharule anasema kijiji hicho kimepewa jina la chifu huyo ambaye alitokea nchini Afrika ya kusini na kutawala ungoni kuanzia mwaka 1847 hadi 1889 alipofariki na kuzikwa katika kijiji hicho.
“Chifu Mharule baada ya kufa mwaka 1889 alizikwa kwa taratibu za jadi ya machifu wa Afrika ya kusini,kaburi lake lilikuwa la mviringo,sanda yake ilikuwa ya ngozi ,alikarishwa kwenye kiti cha ngozi,walikamatwa watu wawili wakiwa hai walizikwa naye wakiwa wamesimama mbele na nyuma ya chifu’’,alisimulia mzee Ngonyani.
Amezitaja taratibu za kijadi za wakati huo zilitaka Mfalme au Chifu anapofariki ni lazima azikwe na watu wawili wakiwa hai na kusisitiza kuwa hiyo ilikuwa ni amri ya serikali ya jadi na hapakuwepo mtu aliyepinga.
Mzee Ngonyani amewataja wengi waliokuwa wanazikwa wakiwa hai na Mfalme ni wale ambao walikuwa wamezoeana na kufanyakazi naye kwa karibu.
Hata hivyo amesema kaburi hilo linatumiwa na wananchi wa kijiji hicho kwenda kuhiji kila mwaka kwenye kaburi hilo ambalo lipo kilometa mbili toka kijijini hapo na kwamba ndugu wa Chifu Mharule toka Afrika ya Kusini huwa wanafika kufanya matambiko kwenye kaburi hilo.
Amesema mwaka juzi ukoo wa Mharule toka Afrika ya kusini walifika kushuhudia kusimikwa kwa Chifu Nkosi Imanuel Zulu Gama wa Tano ambaye ndiyo chifu wa wangoni wa sasa.
Machifu watano wa kabila la wangoni ni Nkosi Mharule Zulu Gama alifariki mwaka 1889,Nkosi Mputa Gama ambaye alinyongwa na wajerumani mwaka 1906,Nkosi Usangila Zulu Gama aliyefariki mwaka 1941,Nkosi Korofindo Zulu Gama aliyefariki Dunia mwaka 1949,Nkosi xzavery Zulu Gama alifariki mwaka 2001 na Chifu wa Wangoni wa Tano ambaye anaendelea hadi sasa ni Nkosi Emanuel Zulu Gama.