Magari matatu mapya yaliyonunuliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) yalipowasili Hospitalini hapo kutokea Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika akiongea na watumishi wa Hospitali hiyo wakati wa tukio la kupokea magari matatu mapya kwa ajili ya Hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika akipokea kadi za magari matatu mapya kutoka kwa mkuu wa kitengo cha Ugavi Hospitalini hapo, Hellena Chitukuro wakati wa kupokea magari matatu mapya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika, akionyesha moja ya kadi za magari mapya yaliyonunuliwa na Hospitali hiyo kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya, anayeangalia ni Mkurugenzi wa Utawala wa Hospitali hiyo, Neema Tawale.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika, akiingia katika moja ya magari matatu yaliyonunuliwa na Hospitali hiyo ili kwa ajili ya kulijaribu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika, akijaribu moja ya magari mapya yaliyonunuliwa na Hospitali hiyo kwa ajili kuimarisha huduma za afya.
……………
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH) imepata gari mpya tatu yenye thamani ya jumla ya zaidi ya Sh milioni 335.145 ambayo yataisaidia hospitali hiyo kutoa huduma ya afya ikiwamo na kutekeleza programu ya huduma mkoba kwa maeneo ya vijijini mkoani Dodoma.
Hospitali ya Benjamin Mkapa ilianzisha programu ya huduma mkoba ya kufikisha huduma za afya za kibingwa kwa wananchi wa vijijini mkoani Dodoma ikiwa ni katika kutimiza lengo la Serikali ya Awamu ya Tano yenye kuhakikisha inajenga taifa lenye watu afya njema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk Alphonce Chandika alisema magari hayo mapya yatasaidia huduma za afya na kuwezesha mpango kutoa huduma kwa jamii ya watanzania walioko vijijini
Alisema pia yatasaidia katika kutekelezaji wa suala zima la uchangiaji damu wa Hospitali hiyo ambao utaanza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa benki ya damu mapema mwaka ujao.
” Katika kuendela kuimarisha huduma katika hospitali yetu tuko katika mchakato wa kujenga benki ya damu ambayo inatarajia kukamilika mapema mwakani, hivyo kupatikana kwa magari haya kutatusaidia katika utekelezaji wa mpango wa kuchangia damu,” alisema.
Dk Chandika aliongeza: “magari hayo yataiwezesha BMH kwenda mashuleni na katika taasisi mbalimbali ili kuhamasisha wananchi na umma wa watanzania kujitolea damu ambayo itahifadhiwa kwenye benki ya damu ya hospitali.
Dk Chandika alisema ukusanyaji wa damu utakaofanywa na hospitali hiyo utasaidia katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu katika mikoa ya Kanda ya Kati.
” Kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya damu katika mikoa ya Kanda ya Kati kwasababu ya ongezeko la watu katika Mkoa wa Dodoma na benki ya damu ya hospitali ya Mkoa (General) haiwezi haiwezi kukidhi mahitaji. Benki yetu ya damu itasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa damu,” aliongeza.
Ujenzi wa benki ya damu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo kwa sasa iko katika hatua za mwisho, utakuwa na umuhimu zaidi wakati wa kuanza utoaji wa huduma ya kupandikiza uboho inayotarajia kuanza kutolewa hospitalini hapo mwakani.
Dk Chandika alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kuwezesha Hospitali ya Benjamin Mkapa kupata magari hayo, huku akiwataka wafanyakazi wa Hospitali hiyo kutunza ili yatumike kwa muda mrefu jambo ambalo litasaidia kutimiza wajibu wa hospitali wa kutoa huduma za afya kwa ufanisi.