Na WAF- DOM.
NAIBU WAZIRI wa afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa viongozi ngazi ya mkoa na Wilaya kushirikiana kwa kwa karibu kusimamia takwa la kisera linaloelekeza huduma bure kwa watoto chini ya miaka mitano na wajawazito.
Dkt. Mollel amesema hilo leo Februari 7,2023 wakati akijibu swali la Mhe. Dorothy Kilave katika Mkutano wa kumi kikao cha sita, Bungeni Jijini Dodoma.
“Swala hili ni swala la kisera kwamba, mama mjamzito na watoto wa umri chini ya miaka mitano hawatakiwi kulipishwa, hivyo niombe Wakuu wa Wilaya na Wakauu wa Mikoa tuweze kushirikiana kwa pamoja kusimamia hili takwa la kisera.” Amesema Dkt. Mollel.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba licha ya changamoto ya msongamano wa idadi kubwa ya watu wanaohitaji huduma katika vituo vya afya hali inayopelekea upungufu wa baadhi ya mahitaji ya huduma hizo.
Ameendelea kusema kuwa, tayari Serikali imeiboresha MSD na sasa inatarajia kuwa na maoteo mazuri ya uhitaji wa dawa na vifaa tiba kulingana na idadi ya watu wanaohitaji huduma katika vituo hivyo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, kwa vituo vya binafsi visivyo na ubia na Serikali na vya Serikali suluhu ya hili ni ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utakapopitishwa utasaidia mwananchi kupata huduma zote kwa ngazi zote bila malipo kuanzia Zahanati mpaka hospitali ya Taifa.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel ameiagiza Hospitali zote na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha wanamhumia mtoto yoyote ataezaliwa njiti bila usumbufu, huku akisisitiza kuwa endapo hatakuwa kwenye Bima atahudumiwa bure pia kama Sera ya afya ya mwaka 2007 inavyoelekeza.