Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe.Jaffar Haniu ameongoza zoezi la Upandaji miti katika Kijiji Cha Ijoka kata ya Mpombo Halmashauri ya Busokelo ikiwa ni hatua muhimu ya kulinda vyanzo vya maji, kudumisha uoto wa asili, na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Jumla ya miti 1000 imepandwa Leo katika eneo hilo huku malengo yakiwa ni kupanda miti 1,500,000 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho Mhe.Haniu ameagiza wakazi wa eneo hilo kuhakikisha wa wenapanda miti mara kwa mara sambamba na kuepukana na tabia ya ukataji miti hovyo, kuchoma moto, kulima kando ya vyanzo vya maji na kuchunga Mifugo kwenye hifadhi za maji.
Aidha amewahakikishia wakazi wote wa Wilaya ya Rungwe kuwa Mbolea ya Ruzuku imeendelea kusambazwa katika maeneo yote kwani Serikali kupitia Wizara ya kilimo imeboresha mazingira ya Kilimo na hivyo kila Mkazi atapata pembejeo hiyo muhimu kwa Maendeleo endelevu nchini.
“Niagize kila kata kuwe na ratiba maalumu inayoonesha ni lini mbolea inaletwa katika kata husika ili kuwaondolea adha wananchi kufuata huduma umbali mrefu huku wakipoteza muda mwingi wa uzalishaji” Ameagiza Mhe.Haniu
Pamoja na hiyo ameagiza mawakala wote wa usambazaji wa Mbolea kuacha kuuza mbolea kwa magendo kwani kufanya hivyo kunaondoa nia njema ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha watanzania wanazalisha kwa tija na Maendeleo bila vikwazo vyovyote.
Katika hatua nyingine Mhe Haniu ametoa maelekezo kwa wazazi wote kuhakikisha watoto wao waliofikisha umri wa kwenda shule sambamba na kujiunga na kidato kwanza wanawapeleka mapema kwani kufanya hivyo itasaidia kupata huduma hiyo muhimu kwa Ustawi wa Mtoto.
Halmashauri ya Busokelo imeandikisha watoto wa darasa la kwanza na wali kwa zaidi ya asilimia 100% huku uandikishaji ukiendelea.