
**********
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wameishauri kamati ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kupeleka mapendekezo maoni ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.
Itakumbukwa kwamba, Mnamo tarehe06 mwezi Januari 2023 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Othuman Chande na Makamu Mwenyekiti Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Yohana Sefue.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza malalamiko miongoni mwa wadau.
“Pendekezo hilo litasaidia kamati kuja na taarifa yenye wigo mpana wa mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla”
Aidha aliishauri kamati hiyo kupitia upya mfumo wa upepelezi kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Pia aliishauri kamati kuweka kipaumbele cha kuboresha sheria Sheria yaKudhibiti Madawa ya Kulevya, Sheria ya Taasisiya Kudhibitina Kupambanana Rushwa, Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi, Sura 200, Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramuwa Binadamu, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari n.k
Ili kuimarisha mfumo wa taasisi za haki jinai na kuweka taasisi zake kuwaza kikatiba, Henga alishauri kutenganishwa kwa majukumu ya Taasisi au mamlaka zinazohusika na haki jinai ikiwemo mamlaka ya kupambana na madawa ya kulevya nchini kufanya kazi za kisera, elimu kwa umma, utaalamu na intelijensia pekee.
“Tofauti na sasa, mamlaka hii imepewa majukumu ya kipolisi ikiwemo kazi za upekuzi, upelelezi na ukamataji, ni busara jukumu la ukamataji ,upekuzi na upelelezi ukabaki kuwa jukumu kuu la jeshi la polisi”
Aidha alishauri kuundwa kwa chombo huru kitakacho shughulikia na mwenendo na utendaji kazi wa jeshi la polisi nchini.
Pia alishauri mahakama kuwa mamlaka ya kutoa dhamana kwa makosa yote kwa masharti na taratibu maalum kulingana na mazingira ya kesi lakini pia kuondokana na adhabu ya kifo kwani adhabu hiyo inatweza utu, ya kikoloni na hatekelezeki.
