Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Chama Cha Walimu Tanzania leo kimekabidhi mifuko 300 ya saruji kwa halmashauri ya jiji la Dodoma, yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni nne laki sita na elf hamsini(4,650,000) kwa ajili ya kuiendeleza miondombinu ya shule, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miondombinu ya elimu.
Akikabidhi mifuko hiyo kwa Meya wa Jiji la Dodoma Davis Mwamfupe, kwa niaba ya Walimu, Katibu CWT Taifa, Deus Seif, amesema wameamua kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miondombinu ya elimu hapa nchini.
Amesema kwa mujibu wa kauli mbiu ya chama Cha CWT, ni “Wajibu na haki” hivyo wameona ili kuhakikisha elimu inaboreshwa na wao ni wajibu kuwa sehemu ya maboresho hayo na kuhakikisha Walimu wanakuwa katika sehemu salama katika kufundisha.
“Sisi Kama chama cha walimu ni Wajibu wetu kutoa mchango katika maendeleo ya elimu hapa nchini kama Moto wa chama chetu “Wajibu na haki” kwahiyo hapa tumetimiza Wajibu na kuhakikisha miondombinu ya elimu inaboreshwa” amesema Seif.
Amesema wataendelea kushirikiana na wadau wengine wa elimu katika kuhakikisha miondombinu ya elimu inaboreshwa na wanatambua kuwa kukiwa na miondombinu mizuri hata Walimu watafundisha kwa moyo na kuleta matokeo chanya.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya wananchi ya Jiji la Dodoma, Meya ya halmashauri ya Jiji la Dodoma Davis Mwamfupe amewashukuru CWT kwa kuamua kuleta msaada katika jiji la Dodoma na si maeneo mengine.
Amesema kitendo walichofanya CWT kiwe ni ufunguo kwa mashirika na taasisi nyingine kuunga mkono juhudi za kuboresha miondombinu ya elimu hapa nchini ilikuhakikisha elimu inaboreshwa hapa nchini.
Ameelekeza mifuko hiyo ya saruji ielekezwe katika eneo moja na sio kugawa kwa shule zote kwa sababu matokeo hayataonekana, hivyo ameelekeza ipelekwe katika eneo moja ili matokeo yaonekane, na ameagiza kazi itakayofanyika matokeo yapelekwe CWT ili wajue kazi iliyofanyika.
Nae Afisa Elimu Msingi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mabeyo, amebainisha kuwa kwa upande wa Jiji mahitaji ya vyumba vya Madarasa ni 1522, wakati vilivyopo ni 916 tu, kwa upande wa matundu ya vyoo vya wanafunzi wa kiume mahitaji ni 1936, huku yalivyopo ni 506, na upande wa kike mahitaji ni 2456 na yaliyopo ni 577 tu.