.,……………………..
Na Sixmund Begashe
Serikali imetoa wito kwa wananchi waendelee kutumia bidhaa za misitu zilizotengenezwa hapa nchini kutokana na bidhaa hizo kuwa imara, zinazodumu muda mrefu na zenye gharama nafuu.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, alipokua akizungumza na Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Misitu ( NAFAC).
Mhe. Balozi Dkt. Chana amesema dhamira ya Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuiona sekta ya Misitu ikipiga hatua na kuwanufaisha zaidi Watanzania hivyo Wizara anayoiongoza itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo kwa lengo la kuzalisha bidhaa bora zinazotokana na Misitu ili wananchi wapate bidhaa bora na fursa za ajira.
Ameipongeza Kamati hiyo kwa kazi nzuri inayoifanya ya kuishauri Wizara kwenye Masuala ya Misitu huku akieleza kuwa taarifa iliyowasilishwa na kamati hiyo kuhusu Sekta ya misitu itaisaidia Wizara kuimarisha utendaji na kufanya maboresho kwenye sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Misitu (NAFAC) Prof. Shaban Chamshama akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati hiyo ameushukuru uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana vyema na Kamati hiyo kwa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake.
Kikao hicho cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati hiyo ya Kitaifa ya Ushauri wa Misitu, kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka, Naibu Katibu Mkuu Bw. Juma Mkomi, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki Bw. Deusdedith Bwoyo na baadhi ya Wataalam wa Misitu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.