Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Holle Makungu, akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26, 2023 Jijini Dar es Salaam.
…………………
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Watu wawili Wakazi wa Manispaa ya Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam wamehukumiwa kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kutoa rushwa ya Shilingi Laki nane (Sh. 800,000) kwa Askari wa Jeshi la Polisi DC Hamis Masana wa kituo Cha Polisi Kigamboni kitendo ambacho ni kinyume kifungu Cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/ 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Holle Makungu, amewataja watu hao kuwa Bw. Hamis Hamisi pamoja na Abdalah Ngoma ambapo wamehukumiwa na Mahakama ya Wilaya Kigamboni baada ya kukili makosa yao.
“Januari 23, 2023 tulipokea taarifa kuna wananchi wanamshawishi Askali wa Jeshi la Polisi wa kituo Cha Kigamboni kwa ajili ya kumpatia kiasi cha Shillingi Laki nane ili aweze kumwachia huru ndugu yao aliyekamatwa kwa tuhuma za kukutwa na kiasi kikubwa cha bangi” Bw. Makungu
Bw. Makungu amefafanua waliifanyia kazi taarifa hiyo na kuweka mtego uliandaliwa na kuwanasa watu hao wakati wakitoa rushwa na kufishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.
Amesema kuwa Watuhumiwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Evelyn Daimon siku ya tarehe 25/1/2023 na kufunguliwa shauri la Jinai namba CC.8/2023 mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Is – Haq Bakari Kuppa.
Ameeleza kuwa watuhumiwa wote wawili walikiri makosa yao ambapo walihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi Laki sita.
“Washtakiwa wote walipelekwa kuanza kutumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini na fedha shilingi lakini nane za rushwa iliamuliwa kuingizwa Serikalini kupitia Idara ya Mahakama” amesema Bw. Makungu.
Ametoa rai kwa watumishi wa umma kuiga alichokifanya askari huyo, kwani tafiti zinaonyesha kuwa watoa rushwa ni wengi ila taarifa hazitolewi kwakuwa baadhi ya watumishi wenye dhamana wamekuwa wabinafsi kwa kupenda kujineemesha wenyewe kwa kupokea fedha tusizo stahili na kujisahaulisha viapo vya uadilifu.
“Nitumie nafasi hii kutoa onyo kwa wananchi wenye fikra za kutoa rushwa kwa watumishi wa umma, kutoa rushwa ni kosa chini ya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007 na hivyo tutaendelea kuwakamata wale wote wanaotoa sawa na tunavyowakamata wanaopokea.