Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Mwenyekiti wa kikao hicho Abdalah Mtinika akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Temeke cha Robo ya Pili ya Mwaka ambacho kimefanyika leo.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Dkt Irine Haule akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Temeke cha Robo ya Pili ya Mwaka ambacho kimefanyika leo
………………….
NA MUSSA KHALID
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es salaam imejipanga kuendelea kukusanya mapato kwa bidii Ili kuweza kuongeza ufanisi zaidi katika utekelezaji miradi mbalimbali na utoaji wa huduma katika Manispaa hiyo.
Pia imeelzwa kuwa Manispaa hiyo katika Mwaka wa Fedha wa 2022/2023 wamejipanga kukusanya kiasi cha Shilingi Bill 43.3 kwa mapato ya ndani ambapo mpaka sasa kwa taarifa za Disemba Mwaka jana tayari wamekusanya Bill 22 sawa na asilimia 51.4.
Hayo yameelezwa leo katika kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Temeke cha Robo ya Pili ya Mwaka ambapo Mstahiki Meya na Mwenyekiti wa kikao hicho Abdalah Mtinika ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kutokana na kuwapatia Fedha kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Madarasa.
‘Asilimia kubwa baraza letu la leo Waheshimiwa madiwani wamezungumza sana suala la miundombinu na hasa barabara kwani ndio tunaamini ndio kilio cha wananchi hivyo ni matumaini yetu kuwa barabara zote zitakwenda kukamilishwa kwa wakati’amesema Meya Mtinika
Mtinika amewataka wananchi kuendelea kumuunga Mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani amewaletea miradi mbalimbali ambapo katika upande wa serikali imewapatia kiasi cha Shilingi Bill 4 na Milioni miamoja na arobaini kwa lengo la kujenga madarasa 207 ambayo mengi yamekamilika kwa asilimia 99.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Dkt Irine Haule amesema kuwa Halmashauri hiyo ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma wamejipanga kuendelea kukusanya mapati kwa wingi.
‘Kama Manispaa ya Temeke sisi tumejidhatiti na tuko tayari kuendelea kukusanya mapato ili wananchi waweze kupata huduma ambazo wanatarajia kuzipata katika manispaa yetu’amesema Dkt Haule
Kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara Dkt Haule amesema Manispaa hiyo kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 imetenga kiasi cha zaidi ya Sh Bill 3 kwa ajili ya maboresho ya barabara.
Nao baadhi ya wajumbe wa Baraza la Madiwani ambao wameshiriki kwenye kikao hicho akiwemo Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu Maanya Juma Maanya wamesema wataendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluh Hassan katika kuhakikisha wanasimamia utekeleza wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo iwewe kukamilika kwa wakati