Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema lengo la Bima ya Afya kwa Wote ni kuchangiana kwa gharama za matibabu kwa wananchi wote ikiwemo wale ambao hawana uwezo ambao kwa kiasi kikubwa ndio wanaohangaika kutafuta huduma za matibabu wanapougua.
Waziri Ummy amesema hayo leo tarehe 23 Januari 2023 wakati alipokutana na Wahariri wa Vyombo vya habari pamoja na Wakurugenzi wa taasisi mbalimbali katika kikao cha kujengewa uelewa kuhusu Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote kilichofanyika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar Es Salaam.
Waziri Ummy amesema kuwa asilimia 15 tu ya watanzania ndio wamejiunga na kunufaika na bima afya ambapo asilimia 99 wamejiunga na bima wakati wakiwa wagonjwa kitu kinachoondoa dhana ya bima kwani mtu anatakiwa ajiunge kabla ya kuugua.
“Japo muswada huu unapendekeza kila mtanzania ajiunge na bima ya afya kwa kufungamanisha na baadhi ya huduma za kijamii lakini hakuna mtu atakayekamatwa kwa kuwa hajajiunga na bima ndio maana serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kila mtanzania kuwa na bima ya afya na kuweza kujiunga ili kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua”. Ameongeza Mhe. Ummy.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii ili kujenga uelewa mpana wa umuhimu wa kila mwananchi kuwa na bima ya afya kama nyenzo itakayomsaidia kupata matibabu wakati wote bila kujali hali yake ya kipato kwa wakati huo.
Prof. Makubi ameongeza kuwa pamoja na kutoa elimu, Wizara imeendelea pia kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali na kufanya maboresho katika maeneo hayo, kwa mfano katika eneo la ufungamanishaji baada ya kupokea maoni baadhi ya maeneo yamepungua kutoka tisa hadi kufikia matano.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo kuhusu Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Mkurugenzi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Benard Konga kwa niaba ya kamati inayoratibu muswada huo, ametaja baadhi ya huduma ambazo wananchi watakazonufaika nazo ikiwemo ada ya kuandikisha na kumuona daktari, gharama za vipimo, dawa na gharama za kulazwa.
Huduma zingine ni gharama za dawa zote kama zilivyoainishwa katika orodha ya taifa ya dawa muhimu (NEMLIT), gharama za upasuaji mdogo, mkubwa na ule wa kitaalamu zaidi unaofanywa na madaktari bingwa, huduma ya afya kinywa na meno, huduma za matibabu ya macho, vifaa saidizi (medical/ othopaedic appliances) na huduma ya mazoezi ya viungo.
Naye, Msemaji Mkuu na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Gerson Msigwa amesema waandishi wa habari ni watu muhimu sana katika kutoa elimu na kuwaomba kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa bima hii kwa watanzania na kuongeza kuwa bima hii inakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto za matibabu kwa watanzania.
Akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Bw. Deodutus Balile amemhakikishia Mh. Waziri kuwa watatoa elimu kuhusu umuhimu wa bima hiyo, na kuomba pale watakapohitaji wataalam kutoa ufafanuzi watoe ushirikiano ili lengo la kutoa elimu liweze kufanikiwa.