Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul Januari 18, 2023 ameagiza wananchi na Taasisi zinazozunguka maeneo ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kuyatunza na kuyalinda ili yasipoteze asili yake.
Naibu Waziri Gekul, ametoa maelekezo hayo katika ziara aliyofanya katika Kambi za Wapigania Uhuru za Dakawa na Mazimbu Mkoani Morogoro.
Akiwa katika eneo la Dakawa aliagiza Taaisisi zilizopo chini ya Kituo Cha Dakawa kuanzisha mpango wa Matumizi ya Ekari 4000 ambazo hazitumiki au vinginevyo ziwasilishwe katika Mamlaka nyingine kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo.
“Jukumu la kutunza maeneo haya ni letu sote, sisi Wizara yenye dhamana Kwa sasa tumeanza mpango wa kuyatambua kwa kuyawekea alama , pamoja na kukusanya nyaraka mbalimbali na kuzihifadhi katika maktaba ili zisipotee” amesema Mhe.Gekul.
Akiwa katika Kambi ya Mazimbu, ametumia nafasi hiyo kuwagiza Maafisa Utamaduni nchini, kukusanya historia ya Utamaduni katika maeneo hayo ili yatambulike na yatumike kwa shughuli za Utalii wa Utamaduni.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika Bw. Boniface Kadili amesema Kituo kimeendelea kupokea fedha za Ukarabati wa maeneo mbalimbali ya Kambi hizo, ambapo amesema wanaendelea kukarabati jengo la Makao Makuu lililopo Dar es Salaam na baadhi ya Kambi za wapigania uhuru hao.
Katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Alhaj Majid Mwanga pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Alberto Msando, ambao wote wameahidi kutunza na kulinda maeneo hayo.