Sabina Barma (28) mwenye watoto watano ameuawa kwa kuchomwa shingoni kwa kitu chenye ncha Kali na mtu anayetajwa kuwa ni mumewe.
Marehemu ameacha watoto watano wa mwisho akiwa ana umri wa Mwaka mmoja ambaye alikutwa akinyonya ziwa la mama yake bila kujua kuwa alishafariki dunia.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Gisigisi Kijiji Cha Saydoda kata ya Ufana Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara John Masong Manonga amesema tukio hilo lililotokea Januari 14, 2023 kijijini hapo limewastua wengi kwani marehemu alikutwa akiwa na majeraha shingoni.
Wananchi wa kitongoji cha Gisigisi wameiomba serikali imtafute mtuhumiwa na kumchukulia hatua stahiki ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ovu kama hiyo.
Inaelezwa na Mmoja wa mashuhuda kuwa mwanamke huyo alikuwa amefungwa mikono na kuteswa na kuchomwa shingoni kwa kitu chenye ncha kali na maeneo mbalimbali ya mwili wake, kwa kuwa marehemu alikutwa na kamba mkononi.
Mume anayetuhumiwa kutekeleza mauaji hayo aliyetajwa kwa jina Moja la Nada, waliyezungumza naye wanasema walimpigia simu lakini alijibu yupo safarini na baadaye simu yake iliiita bila kupokelewa.
Wazazi wa marehemu wamesema baada ya tukio hilo wameitenga familia hiyo na kuamua kuuchukua mwili wa Mtoto wao na kwamba watamzika wenyewe nyumbani kwao na kuwachukua watoto wote kuishi nao.