KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda amesema kuwa vyombo vya habari vikiwa huru vitaaminika kwa jamii kutokana na kutoa maudhui ambayo yanatija kwa jamii.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,Sheikh Ponda alisema kuwa vyombo vya habari vitasaidia kutoa elimu kwa jamii kutokana na aina ya habari ambazo watakuwa wanaziwasilisha kwenye vyombo vyao vya habari.
Alisema kuwa vyombo vya habari vikiwa huru vitawasilisha fikra za wananchi na kuisaidia serikali kujitathimini juu ya mwenendo wa uongozi wao kutokana na aina ya habari ambazo wananchi watakuwa wanaziwasilisha kwa jamii kupitia vyombo vyao vya habari.
Sheikh Ponda alisema kuwa demokrasia itakuwa sana kutokana na vyombo vya habari kuwa huru kuandika ukweli uliopo nchini kutokana siasa ambazo zinakuwa zinaendelea wakati huo.
Alisema kuwa vyombo vya habari vikiwa huru uchumi wa nchi utakuwa kutokana na waandishi wa habari kueleza ukweli namna ya hali ya uchumi ilivyo kwenye jamii hivyo lazima watawala watachukua hatua juu ya kuukuza uchumi.
Sheikh Ponda alisema kuwa vyombo vya habari vikiwa huru malengo ya vyombo vya habari yatafikiwa kutokana na uhuru uliopo na kufanikisha kuwa kiungo baina ya wananchi, taasisi binafsi na serikali kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo ya wananchi.
Aidha sheikh Ponda alisema kuwa mahusiano ya kimataifa yatakuwa kwa kiasi kikubwa kutokana na uhuru wa vyombo vya habari na kusaidia watanzania waliopo nje ya nchi kupata taarifa sahihi za maendeleo ya uchumi na demokrasia ya nchi yao.