Bi. Dorothea Clemence Kipangula Mkufunzi Msaidizi katika Kampasi ya SUA Mizengo Pinda akizungumza na SUAMEDIA faida za mafunzo hayo mara baada ya kuhitimishwa Chuoni hapo.
Mwalimu wa TEHAMA Bi. Neema Mwawadu akizungumzia mafunzo hayo nje ya Ukumbi wa Mkatano wa Kampasi ya SUA Mizengo Pinda Mkoani Katavi.
Makamu Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi SUASO Kampasi ya Mizengo Pinda bwana Abihudi Fadhili akizungumza na SUAMEDIA kwa niabaya Wanafunzi wengine Umuhimu na faiza za mafunzo hayo kwao.
Na: Calvin Gwabara – Katavi.
Wanataaluma na Wanafunzi katika Kampasi ya SUA Mizengo Pinda Mkoani Katavi wameupongeza Mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) kwa kuwezesha na kuhimiza elimu ya masuala ya Jinsia katika Taasisi za Elimu Chuoni kwakuwa inasaidia kufanya mazingira ya Chuo kuwa salama kwa wote.
Akionge mara baada ya mafunzo hayo Mkufunzi Msaidizi katika Kampasi hiyo Bi. Dorothea Clemence Kipangula amesema mara nyingi watu wamekuwa wakidhani Jinsia ni mambo yanayohusu Mwanaume na Mwanamke pekee lakini baada ya mafunzo hayo amemejifunza kuwa Jinsia inakwenda mbali na kuwajumuisha watu wenye ulemavu na mahitaji maalumu.
“Kwahiyo mimi kama Mwalimu nimejifunza kuwa hata ninapokuwa nafundisha hasa linapokuja kundi jipya la Wanafunzi mimi kama mwalimu natakiwa kuchukua muda kuwatambua vizuri na kujua ni Mwanafunzi gani anauhitaji maalumu na nitamfundisha vipi ili aweze kupata kile anachokitarajia sawasawa na wengine na kutimiza ndoto na malengo yake Chuoni” Alifafanua Bi. Dorothea.
Aidha amesema kwa mafunzo hayo yamewafungua macho kama Walimu namna ya kuteleza majukumu yao lakini pia katika maisha yao ya kawaida na kusaidia kujenga Chuo na Wahitimu wanaotoka katika Kampasi ya Mizengo Pinda na SUA kwa ujumla wake.
Nae kwa upande wake Mwalimu Neema Mwawadu amesema amefurahishwa na mpango wa Wizara na Chuo kuanzisha Dawati la Jinsia ambalo litakuwa linashughulikia maswala yote ya Unyanyasaji na Ukatili wa kijinsia pamoja na kutoa Elimu sahihi ya masuala hayo ambayo yasipodhibitiwa yanaweza kuathiri utekelezaji wa majukumu kwa Walimu, Wanafunzi, Wafanyakazi wengine pamoja na watoa huduma Chuoni hapo.
“Mafunzo haya yatanisaidia sana maana kwanza nafundisha wanafunzi wa Kike na Kiume hivyo wakati nikiwa darasani nitahakikisha hata kwenye kutoa mifano sitoi ambayo inaweza kuathiri kundi lolote ili kila mmoja ajifunze kwa amani na kuona anathaminiwa” alisisitiza Bi. Neema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi SUASO Kampasi ya Mizengo Pinda bwana Abihudi Fadhili amesema wamefurahi sana kupata mafunzo hayo ambayo yameelezea Jinsia kwa mapana yake na hivyo kuwezesha kujua makossa ambayo wamekuwa wakiyafanya kutokana na matendo yao ambayo wanayafanya kwa kufahamu au kutokufahamu kuwa ni makossa na kuathiri maisha ya watu wengine.
“Tumeona ni muhimu kujifunza masuala haya maana itatusaidia kuondoa migogoro mbalimbali kati ya Walimu wetu na Wanafunzi na Wanafunzi, Wanafunzi na Wafanyakazi Lakini pia Wanafunzi na Watoa huduma Chuoni na nitahakikisha nakuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wenzangu wote kwenye Kampasi yetu ya Mizengo Pinda” alieleza bwana Abihudi.
Mradi wa Elimu ya Juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) umewezesha wataalamu na wabobevu wa Masuala ya Jinsia kufanya mafunzo ya kujenga uwezo kwa Wanataaluma na Wanafunzi kwenye kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi ili kuwaandaa utekelezaji wa Sera na Miongozo mbalimbali ya Chuo, Wizara na Kikanda katika kushughulikia masuala yote ya Jinsia na hivyo kufanya taasisi za Elimu kuwa salama kwa wote.