Mkuu wa Wilaya ya
Singida Mhandisi Paskas Muragili (katikati) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida akiwasha kifaa maalumu cha kupiga king’ora kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi mpya wa kusambaza umeme kwenye Vijiji Miji viliyopo pembezoni mwa Manispaa ya Singida katika hafla iliyofanyika Kata ya Mwankoko Desemba 29,2022 ambao utagharimu Sh. 7.11 Bilioni zilizotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) amapo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakuwa msimamizi wa mradi huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua mradi mpya wa
kusambaza umeme kwenye Vijiji Miji viliyopo pembezoni mwa Manispaa ya Singida ambao
utagharimu Sh. 7.11 Bilioni na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakuwa
msimamizi wa mradi huo.
Mradi huo wa kusambaza umeme katika
Vijiji Miji (Peri-urban Electrification)
ambao umezinduliwa Desemba 29, 2022 Kitongoji cha Kitope Darajani Kata
ya Mwankoko utatekelezwa kwenye vitongoji 34 vilivyopo katika Kata 9 ambapo wateja watarajiwa
ni zaidi ya 2000.
Akizindua Mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya
Singida Mhandisi Paskas Muragili aliwaomba wananchi wachangamkie mradi huo kwa
kuanza kusuka nyaya za umeme katika
nyumba zao ili waweze kufungukiwa kwa gharama ya Sh.27,000.
“Mradi huu ukikamilika unakwenda kubadilisha uchumi wa wanananchi
kwani watautumia umeme huo kuanzisha viwanda vidogo na shughuli zingine za uzalishaji ambazo
zitatumia nishati hiyo hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa
ujumla” alisema Muragili.
Muragili alimuomba mkandarasi wa mradi huo kuukamilisha ndani ya mwaka
mmoja badala ya miezi 18 aliyopewa
kuukamilisha kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuchelewa kuukamilisha
ndani ya muda huo kwa kuwa unatekelezwa kwenye maeneo yenye miundombinu mizuri
ya barabara.
Akifafanua kuhusu Mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Nicolaus Moshi alisema
mradi wa usambazaji nishati ya umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji
kwa hapa nchini Mkoa wa Singida ndio wanaupata kwa mara ya kwanza.
Alisema mradi huo utajenga jumla ya kilomita 40.5 za msongo wa kati na
msongo mdogo na kupitia mradi huo watafunga mashine umba au Transfomer 33 katika
vitongoji vilivyotajwa na kuweza kuwaunganishia wateja wa awali 1802 ambapo
aliwaomba wananchi wa maeneo utakapo pita mradi huo kuchangamkia fursa hiyo.
Moshi alisema REA imekuwa ikitekeleza miradi mingine mingi hapa nchini Mkoa
wa Singida ukiwa ni moja ya mikoa ambayo inanufaika na miradi hiyo na akatumia
nafasi hiyo kumtambulisha kwa wananchi na mgeni rasmi Mkandarasi wa Kampuni ya Central Electricals International Ltd
anayetekeleza mradi huo na kukabidhiwa rasmi mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya
ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili ili aanze kufanya kazi .
Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali walipata fursa ya kutoa salamu huku
wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo
na mingine mingi na wito wao mkubwa wakiomba wananchi kutunza miundombinu ya
mradi huo na kuwataka wachangamkie umeme huo kwa kuanzisha miradi ya kuinua
uchumi wao.
Baadhi ya viongozi waliopata fursa ya kutoa salamu ni Mwenyekiti wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru, Diwani wa Kata ya Mwankoko,
Emmanuel Daniel, Mbunge wa Singida Mjini ambaye aliwakilishwa na Diwani wa Kata
ya Kisaki, Moses Ikaku, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwankoko (A) Jacobo Yohana
na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida,
Yagi Kiaratu. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Nicolaus Moshi (kulia) akimkabidhi faili la mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, Meneja Mradi wa Kampuni ya Central Electricals International Ltd, Pravin Thorat inayo jenga mradi huo. Katikati anayeshuhudia tukio hilo ni Mwakilishi wa Mbunge wa Singida Mjini, Diwani wa Kata ya Kisaki, Moses Ikaku.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwankoko (A) Jacobo Yohana akizungumza.