…………………………..
Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement KIVEGALO amewaomba radhi wananchi wa vijiji vya Igando na Kijombe wilayani Wanging’ombe kufuatia kucheleweshwa kwa mradi wa maji waliousubiri kwa muda mrefu.
Mhandisi Kivegalo ameeleza hayo wakati akifanya ziara ya kutembelea Mradi wa Maji Mtiririko kwa Vijiji viwili vya Malangali na Hanjawanu (Igando-Kijombe) Wilayani Wanging’ombe Mkoa wa Njombe.
“Kwa kweli kwanza nitumie nafasi hii kuwaomba radhi wananchi wote kwa kusubiri mradi huu kwa muda mrefu, karibu miaka kumi sasa tangu mradi huu ulipoanza kutekelezwa.” Alisema Mhandisi KIVEGALO.
Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA alifanya ziara mwezi mmoja uliopita na kutembelea mradi huo ambapo hakuridhishwa na ubora wa kazi pamoja na kasi ya utekelezaji wa mradi.
Aliagiza Mkandarasi wa mradi huo kampuni ya M/S STC JV YELL LTD kufanya marekebisho yote na kuhakikisha mkataba wa ujenzi wa mradi huo unazingatiwa ipasavyo.
Ziara hiyo iliyoambatana na wataalamu kutoka RUWASA Makao Makuu imeleta matokeo chanya baada ya Mkandarasi wa mradi kuleta timu yake ya wataalamu na kurekebisha mapungufu yote kama yalivyoelekezwa.
Kwasasa mradi huo upo asilimia 90 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi wa Januari 2023.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya M/S STC JV YELL LTD Allan Makame ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia fedha kwa wakati.
Pia amesema kuwa haidai fedha yoyote serikali ingawa wamefanya kazi kwa asilimia 90 fedha walizoomba ni asilimia 70 tu.
Mradi wa maji wa mtiririko wa Igando Kijombe umesanifiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa vijiji 10 wilayani Wanging’ombe vya Malangali, Wangamiko, Mpanga, Luduga, Hanjawanu, Igando, Iyayi, Lyadebwe, Mayale na Kijombe vyenye wakazi wapatao 14,377.
Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya M/S STC JV YELL LTD kwa gharama ya shilingi 12,437,407,360.00 fedha za ndani kupitia Mfuko wa Maji (NWF).