Wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari kutoka Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA) wametembelea TFS – Shamba la Miti SaoHill ili kujifunza shughuli za uhifadhi zinavyofanyika katika misitu ya kupandwa na namna misitu hiyo inavyosaidia katika uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo wahariri hao wamesema kuwa kumekuwa na dhana tofauti ya uhifadhi wa maeneo ya misitu ya kupandwa kutokana na maeneo hayo kupandwa miti ya kibiashara ambapo inapelekea wananchi kuamini miti hiyo kupunguza kiwango cha maji katika maeneo hayo.
Aidha wamefurahishwa na namna shughuli za uhifadhi wa maeneo ya misitu unavyofanyika kutokana na eneo la Shamba la Miti kuwa kubwa kuliko mashamba yote ya miti ya kupandwa na hivyo kuonesha jitihada kubwa zinazofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania katika maeneo ya misitu.
“MECIRA tunaunga mkono juhudi za serikali kwenye kuhakikisha kwamba tunatoa hamasa na elimu kwa wananchi ili wafahamu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira” Amesema Hamisi Mkotya, Msemaji wa MECIRA
Ameongeza kuwa jukumu la uhifadhi ni la jamii zima ikiwemo wanahabari na hivyo kuwakumbusha TFS kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa kwa jamii ili kuondoa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikififisha juhudi za uhifadhi nchini.
“MECIRA tunaunga mkono juhudi za serikali kwenye kuhakikisha kwamba tunatoa hamasa na elimu kwa wananchi wafahamu umuhimubwa kulinda na kuhifadhi mazingira”
“Lakini si hivyo tu tukasema leo tutembelee katika msitu wa Shamba la Miti la SaoHill iliyo chini ya Wakala wa Huduma za misitu Tanzania – TFS na tumejionea ambavyo mazingira yanavyohifadhiwa na kutunzwa lakini pia tumeona ambavyo si serikali tu bali hata wananchi wanavyofaidika na huduma za misitu, ikiwemo utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwemo chanzo kimojawapo kinachohudumia wananchi zaidi ya 2500 ambao wanazunguka eneo hili la shamba la saohill” Aliongeza Bw. Mkotya
Wameendelea kusema kuwa shughuli mbalimbali za kijamii zimekuwa Chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira ambapo imepelekea uharibifu mkubwa wa maeneo ya misitu.
Naye Kamishna Msaidizi Rasilimali za Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Dr. Abel Masota amesema kuwa jukumu kubwa na TFS ni kuhakikisha misitu yote nchini ambayo ni ya kupandwa na ya asili inasimamiwa ili kuleta uhifadhi wenye tija katika taifa.
Dr. Abel amesema kuwa licha ya changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika maeneo ya misitu ikiwemo suala zima la moto katika misitu lakini TFS imeendela kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii nzima hususani katika masuala mazima ya upandaji miti na utunzaji wa misitu iliyopo.
” Ninawaomba tuendelee kushirikiana katika kuuhabarisha umma kuhusu utunzaji wa Rasilimali za misitu na hii itasaidia wananchi wengi kupitia vyombo vyenu mnavyovisimamia kupata habari kwa usahihi na kwa haraka ambapo itapelekea sasa uelewa wa pamoja katika masuala ya uhifadhi” Amesema Dr. Abel
Naye Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti SaoHill Tebby Yoram wakati wa kuwasilisha taarifa ya Shamba la Miti SaoHill kwa Wahariri hao amesema kuwa licha ya utunzaji wa misitu na vyanzo vya maji TFS kupitia Shamba la Miti SaoHill limekuwa likigawa miche takribani zaidi ya milioni moja katika jamii inayolizunguka shamba hasa katika msimu wa mvua ili wananchi waipande katika maeneo yao na kuhakikisha inatunzwa vyema.
Amesema kuwa ugawaji wa miche unaofanyika umesaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kuwa na uelewa mkubwa katika masuala ya uhifadhi na hivyo kuona thamani kubwa iliyopo inayotokana na uwepo wa misitu ya asili na mashamba ya miti ya kupandwa katika maeneo yao.
Shamba la Miti SaoHill ni miongoni mwa mashamba 24 ya miti ya serikali ya kupandwa yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ambalo lina ukubwa wa hekta 135,903 .