Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa, amewataka viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini katika nyumba za Ibada kuhamasisha Jamii hasa vijana kuhakikisha wanafanya kazi za kujiingizia vipato ili kwenda sambamba na falsafa ya hapa kazi tu.
Mkanwa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Kongamano kubwa la kimataifa lililondaliwa na kanisa la Tanzania Fellowship Churches, linalofanyika Jijini hapa na kushirikisha makanisa yote ya ndani na nje ya nchi, tukio lililoenda sambamba na harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo hapa Dodoma.
Amesema watumishi wa Mungu katika nyumba za Ibada kuwaomba waendelee kuhamasisha Jamii hasa vijana kutafuta kazi za kufanya ili kuhakikisha wanakuwa na vipato na kujikwamua kiuchumi ili waendane na fulsafa ya Rais wetu ya hapa kazi tu.
“Unajua watu wengi hawajaelewa hii falsafa ya hapa kazi tu, lengo ni kuhakikisha kila mtu anakuwa na shughuri ya kufanya kupata kipato, hata neno la Mungu linasema asiyefanya kazi na asile, kwahiyo Watumishi wa Mungu kwenye mahubiri yenu msiache kuhimiza Jamii kuhakikisha wanafanya kazi hasa hawa vijana” amesema Mkanwa.
Amewataka watumishi wa Mungu kuendelea kutoa elimu na kuwaonya hasa jamii kuachana na mambo yasiyofaa hasa mimba za utotoni, mavazi, madawa ya kulevya, rushwa hivi vyote vikemewe kwa nguvu ili tuwe na jamii njema na kwa vizazi vijavyo maana Hali ya Sasa ni mbaya.
Amewashukuru kwa kuendelea kuliombea taifa, pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli kwa kutoa nafasi kwa walio magerezani kwa kosa la uhujumu uchumi kuomba msamaha na kurejesha fedha, na amewataka kutembelea katika magereza kuwahimiza wenye makosa Kama hayo kuomba msamaha.
“Kwanza nimpongeze Rais wetu kwa uamuzi wa kuwataka wenye makosa ya uhujumu uchumi kuomba msamaha, Sasa na ninyi watumishi wa Mungu nendeni huko mkawakumbushe maana kunawengine wamekaa huko mpaka wamechanganyikiwa Sasa muende huko mkawakumbushe waone haja ya kukiri” amesema.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches, Godfrey Malasi, amesema Kanisa hilo hufanya makongamano Kama hayo kila mwaka na kupitia makongamano hayo hupita katika kutoa msaada kama kuisaidia jamii mahospitalini, vituo vya kulelea yatima,magereza na katika mashule.
Amesema na kwa mwaka huu Kongamano hilo linafanyika Jijini Dodoma, na kwa Mkoa wa Dodoma wamepanga kutembelea katika gereza la Isanga na kutoa misaada kwa wafungwa na kuwapa neno la kuwafariji na kuwapa matumaini ili nao wajione bado wanathaminika.
Amesema Kanisa hilo lina utaratibu wa ibada za nyumba kwa nyumba Jambo ambalo linasaidia kuwafikia watu wengi na kueneza neno la Mungu, amesema wanautaratibu wa shule za watoto katika kuhakikisha wanakuwa katika misingi bora na kuja kuwa vijana wenye maadili hapo baadaye.
“Sisi kama watumishi wa Mungu jukumu letu ni kuhakikisha kuwa tunaokoa roho za watu, na kujenga kizazi chenye hofu na kumjua Mungu na kupitia ibada hizi tunawafikia watu wengi na kufundishwa neno la Mungu kwa ukaribu na kwa undani zaidi kupitia ibada za nyumba kwa nyumba” amesema Asikofu Malasi.
Amesema vijana wengi wameharibika kutokana na kutowekewa misingi imara na kufundishwa neno la Mungu tangu wakiwa wadogo, amesema bado kanisa linakazi kubwa ya kuendelea kuokoa roho za watu na kuendelea kutoa maonyo mbalimbali katika nyumba za ibada.