……………………….
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Balozi Dkt. Pindi Chana amewapongeza viongozi na wananchi kutoka katika makundi mbalimbali walioshiriki kupanda Mlima Kilimanjaro wakati wa maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru tarehe 9 Desemba, 2022 akieleza kuwa kitendo hicho ni cha kishujaa na uzalendo mkubwa kwa nchi.
Aidha, Licha ya pongezi hizo ametoa wito kwa kuendelea kuwahamasisha wananchi na wadau mbalimbali kupanda Mlima Kilimanjaro ili waweze kufurahia mandhari na uzuri wa kipekee ya wa mlima huo ambao ni mrefu zaidi Barani Afrika, kupata elimu ya uhifahdi wa Maliasili pamoja na kujifunza zaidi kuhusu Uhuru na historia ya Taifa la Tanzania.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa ukiwemo Mlima Kilimanjaro ili kuweka mazingira rafiki kwa wageni wanaotembelea vivutio hivyo akitoa wito kwa wananchi na Wadau mbalimbali kufaidika na maboresho hayo.
Ikumbukwe kuwa tarehe 5 Desemba ,2022, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana alikabidhi Bendera ya Taifa kwa wapandamlima zaidi ya 200 waliokuwa wakielekea kilele cha Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru.