…………………….
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekipongeza Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuwaandaa wahitimu kwa kuwajengea ujuzi na maarifa katika fani ya sheria kwa ngazi za Stashahada na Astashahada.
Prof. Ibrahim H. Juma ameyasema hayo kwenye mahafali ya 22 ya Chuo yaliyofanyika Chuoni hapo Desemba, 7 2022.
Aidha amesema kuwa wengi wa wahitimu huendelea na ngazi ya juu ya Elimu ya Sheria na huonyesha mafanikio makubwa hii inadhihirisha na kuthibitisha ubora wa Chuo cha IJA.
Aliendelea kwa kusema wahitimu wa Chuo wameajiriwa maeneo mbali mbali kama vile Makarani wa Mahakama; Watendaji wa Vijiji/Mitaa; Makatibu Wasaidizi katika Makampuni ya Mawakili; Wasaidizi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania; Makatibu wa Sheria Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka, Serikali za Mitaa na kadhalika.
Mhe. Prof. Juma aliendelea kuwasihi wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kuibadilisha na kuisaidia jamii pale mtakapopata nafasi na uwezo wa kufanya hivyo kwani sheria inahusika na haki.
“Nawaomba mkawe watu wa haki na wenye kiu ya kutenda haki wakati wote katika yote mtakayoyafanya ili jamii ione utofauti wenu na wengine. Kutenda haki hakusubiri tu hadi uwe mtumishi wa Mahakama au mwajiriwa. Ni zoezi endelevu kwa maisha yetu” Mhe. Prof. Ibrahim H.
Juma aliendelea kuwasisitiza wahitimu hao kwa usemi wa kiingereza usemao “Law is not always the problem. Those who implement the law may be the real problem:” na alifafanua kwa kusema kuwa sio mara zote tatizo huwa ni Sheria au kutokuwepo kwa sheria nzuri, bali sheria inaweza kuwa mbaya pale waliopewa dhamana ya kutekeleza sheria ili itimize malengo wanayotarajia kutoka kwa sheria husika.
Aliwaomba wahitimu wa Mahafali hayo kuwa wasiwe na tatizo katika utekelezaji wa sheria kwani masomo ya Stashahada ya Sheria na Astashahada ya Sheria waliyopata yamewapa mwanga wa kuelewa Sheria ili kuweza kutumia sheria kutatua changamoto zitakazojitokeza.
Mhe. Prof. Ibrahim Juma aliendelea kwa kuwakumbusha wahitimu kutambua elimu waliyonayo kuwa haitoshi kwani kasi ya maboresho na Mabadiliko ya Elimu inatakiwa ilingane na Kasi ya Mabadiliko ya Mahitaji ya Jamii.
“Watanzania wa leo wanaishi katika dunia inayosukumwa na Teknolojia yenye nguvu kubwa ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4IR).
Wahitimu wenye elimu ya ngazi au daraja lolote ni lazima wahakikishe kuwa elimu waliyopata kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama haitoshi ni lazima waiboreshe kila siku ili ilingane na mahitaji ya ushindani mkubwa katika Karne ya 21” alisema Mhe. Prof. Juma.
Kwa upande mwingine, Mhe. Prof. Juma amekielekeza Chuo kwamba, katika awamu ya Pili ya Mradi wa Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (2021-2025), kufanya maboresho ili kiwe Chuo kinachotoa elimu na mafunzo kwa wanafunzi wake na kwa watumishi wa Mahakama kwa kutumia mifumo ya TEHAMA.
Aliendelea kwa kusema awamu ya Pili ya Maboresho ya Mahakama imetenga jumla ya Dola milioni 6 katika eneo la mafunzo ya kuongeza Ujuzi (Skills) na Maarifa (knowledge).
Aidha, Mhe. Prof. Juma amewasihi Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Wahadhiri, Wakufunzi na watumishi wote wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, kujitayarisha na matumizi ya Jukwaa la Ki-elektroniki kutoa mafunzo na elimu kwa waliopo ndani na nje ya Chuo ambapo itaweza kutumika sio tu kwa wanafunzi wa Stashahada na Astashahada ya Sheria, bali pia litatumika kutoa mfunzo Elekezi na Endelevu kwa Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Watendaji, Mahakimu na Watumishi wa kada zote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald A. Ndika aliwakumbusha wahitimu hao 574 kuwa kuhitimu kwao katika ngazi hizo ni mwanzo wa safari ndefu ya kitaaluma.
Hivyo , na kuwaasa waendelee kutafuta elimu bila kuchoka. Mhe. Dkt. Ndika alieleza kwamba kitaaluma wanachuo wa IJA wamekuwa wakifanya vizuri katika vyuo vya elimu ya juu wanapokwenda kwa ajili ya kuendelea na Masomo yao mara tu wanapohitimu IJA, Hivyo kwa ufanisi huo inapelekea wanafunzi hao kuajiriwa katika taasisi mbalimbali za utoaji haki nchini kama vile Mahakama.
Naye Mkuu wa Chuo na Jaji ya Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ameeleza kwamba mpaka sasa Chuo kiko mstari wa mbele katika kutoa mafunzo kwa watumishi mbalimbali wa Mahakama kwa njia ya Mtandao, ambapo mafunzo haya yameweza kuwafikia watumishi wa kada ya Mahakimu na Majaji kwenye maeneo mbalimbali ya utendaji kazi.
Kwa njia ya mafunzo imeweza kupunguza gharama kwa Mahakama ya Tanzania.Mahafali ya 22 ya IJA yameambatana na ufunguzi wa jengo la bweni la wavulana.
Bweni hili lina ghorofa nne na lina uwezo wa kulaza watu 320 na lina thamani ya shilingi za kitanzania billioni 2.6.
Ujenzi wa bweni hili ulisimamiwa na Mahakama ya Tanzania katika mpango wa Maboresho ya Mahakama.