…………………………………
WAKUU wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri zote saba za mkoa wa Singida wamesaini mikataba maalum kwa ajili ya kushughulikia kikamilifu suala la kuboresha lishe katika maeneo yao ikiwa ni utekelezaji wa Agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa hivi karibuni Jijini Dodoma.
Mikataba hiyo inayohusu usimamizi madhubuti wa kuboresha masuala ya lishe katika jamii, imesainiwa na Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa halmashauri mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
“Hivi karibuni, Rais wetu Mama Samia alituita Dodoma na kutuagiza kuongeza jitihada katika kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za lishe bora.” alisema kisha akaendelea;
Nami nimewaita nyie Ma-DC na Ma-DED ili kusaini mikataba hii kwa ajili ya kusimamia lishe bora kwenye maeneo yenu. Nasisitiza, atakayeshindwa jukumu hili atakuwa ametafuta ugomvi na Serikali”
Pamoja na kusimamia huko, Serukamba aliwataka Wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha wanatenga 1,000/- kwa kila mtoto kwenye bajeti ya mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa lishe bora.
“Suala la lishe na afua za lishe tulipe kipaumbele cha kwanza. Tukifanikiwa kuifanya jamii yetu kuwa na lishe bora; hasa kwa watoto wa mwaka mmoja hadi mitano, tutakuwa tumeweka jiwe la msingi kwenye kizazi kijacho,” alisema kisha akaendelea;
Tunaweza tukawa tunajiuliza kwa nini watoto wetu wanafeli sana mitihani tukadhani walimu hawafundishi kumbe sababu mojawapo ni madhara ya kutopata lishe bora; hasa kutoka kwa mama anapopata mimba,” alifafanua.
Wadau mbalimbali wanasema kuwa utiaji saini mikataba hiyo ya kusimamia lishe bora kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri, umekuja wakati muafaka ambapo Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJ-MMMAM) ya miaka mitano iliyoanza Januari 2021.
Mmoja wa wadau hao, Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick alisema kuwa chini ya Programu hiyo ya Taifa inayoshughulika na masuala mtambuka; ikiwemo afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama ni muhimu kwa maendeleo na makuzi ya mtoto chini ya miaka minane.
“Ni dhahiri suala la udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa kundi hilo litakuwa historia. Hivi sasa takwimu zinaonesha udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano limepungua kwa asilimia 10 katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Naamini chini ya juhudi hizi zilizopewa msisitizo na Rais mwenyewe, changamoto hii inaenda kwisha” alisema.
Hata hivyo, Utafiti wa Kitaifa wa hali ya lishe nchini mwaka 2018, unaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Singida wana tatizo la udumavu, asilimia 5 wanakabiliwa na ukondefu na asilimia 15 ya watoto hao wana uzito mdogo.
Daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya Wanawake na Watoto hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani anasema pamoja na sababu nyingine, mara nyingi udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa mtoto ni matokeo ya lishe duni na huleta homa za mara kwa mara.
“Lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo. Hudumaza ukuaji wa kimwili na kiakili lakini pia hupunguza uwezo wa mtoto kufanya vizuri shuleni na ufanisi wa kazi katika maisha ya utu uzima.
Ndio maana msisitizo mkubwa wa lishe bora huwekwa kwa mtoto katika siku 1,000 za mwanzo; yaani tangu mimba kutungwa” alifafanua.
Baadhi ya wazazi na walezi wanasema kuwa cha muhimu ni kwa wataalamu wa afya, lishe na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa jamii; hususan Vijijini juu ya umuhimu wa lishe bora hasa kwa akinamama wajawazito, wanaonyonyesha na wenye watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na viashiria kama vile utapiamlo, umasikini na kukosekana kwa uhakika wa chakula.