Afisa Mtendaji kutoka Kijiji Cha Mlilingwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vicent Clement akitoa taarifa kwa waandishi wa habari hawapopichani wakati walipotembelea kijiji hicho kwa lengo lakukagua miradi inayotekelezwa kupitia mradi wa Mkaa Endelevi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mlilingwa Salum Ally akizungumza katika kikao hicho kilichokutanisha waandishi wa habari na viongozi wa kijiji cha Mlilingwa kata ya Matula mkoani Morogoro na maofisa wa shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA).
Picha zikionesha baadhi ya wajumbe wa kamati mbalimbali za uongozi wakiwemo wanawake na vijana katika kijiji hicho wakiwa katika kikao hicho.
Imeelezwa kuwa Mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa katika Kijiji Cha Mlilingwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro umesaidia kukinufaisha Kijiji hicho katika kukuza usawa wa kijinsia na kusababisha kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wazi katika maamuzi kwa kushirikisha Wanawake na Vijana jambo lilopelekea watu wengi pia hutembelea Kijiji hicho kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali hasa katika utawala bora.
Hii imefanya kijiji hicho kuboresha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo sekta ya Afya,na elimu kutokana na wananchi kuwa na uelewa mpana katika mambo mbalimbali na sasa wanawake kwa vijana wanashiriki katika vikao mbalimbali vya maamuzi ikiwemo upangaji wa mipango ya maendeleo ya kijiji.
Wanawake na vijana pia wamehusika pakubwa katika miradi mbalimbali ukiwemo huu wa “Mkaa Endelevu” na kushirikishwa katika kamati mbalimbali za uongozi na utekelezaji wa miradi utunzaji shirikishi wa misitu ya asili jambo linalowaleta wananchi pamoja ili kufikia malengo ambayo kijiji kimejiwekea kupitia mradi huu.
Afisa Mtendaji kutoka Kijiji Cha Mlilingwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vicent Clement ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari alipotoa taarifa ya mafanikio ya usimamizi shirikishi wa mazao ya misitu Katika kijiji cha Mlilingwa.
Ameongeza kuwa baada ya shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA) na kutoa mafunzo kwa wananchi ndipo Kijiji hicho kilipokoea mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa “Mkaa Endelevu” Julai 7, 2016 na kuanza kuandaa mpango wa matumizi Bora ya ardhi na sheria zake ndogo.
“Baada ya kutenga msitu na matumizi yake Kijiji pia kilitenga na kuandaa mpango wa usimamizi Shirikishi wa msitu na sheria zake ndogo ili kuhakikisha msitu ualindwa na kuhifadhiwa kwa ukamilifu”amesema Clement.
Aidha Afisa Mtendaji Huyo amesema mradi huo pia umetoa Mafunzo mbalimbali Kwa Viongozi na wanakijiji wote yakiwemo Mafunzo ya utawala Bora,Doria na utekelezaji wa Mipango,pia Mafunzo ya uchomaji mkaa kwa njia endelevu,umewasaidia kuelewa namna ya kuchoma kwa njia ya kisasa lakini pia kuunda Umoja wao kupitia vikundi.
Amesema kuwa ili kukabiliana na athari Mabadiliko ya tabia Nchi na kupunguza umaskini mradi huo umetoa mbinu mbalimbali za shughuli za kuijongezea kipato ambapo jumla ya wakulima 48 wamepatia Mafunzo ya Kilimo hifadhi na wanakijiji 90 wamepatiwa elimu ya ujasiriamali.
Kuhusu mafanikio ya mradi huo Afisa Mtendaji Huyo amesema kijiji kimefanikiwa kukusanya kiasi cha fedha Tsh 251,339,500 kwa lengo la kuboresha huduma mbalimbali za kimaendeleo Kijijini hapo ikiwemo huduma za Afya kwa kukarabati zahanati ya Kijiji Pamoja na Ujenzi wa vyumba vya madarasa na Ujenzi wa choo cha kijiji.
Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ) ulikuwa unatekelezwa chini ya Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC) na unatarajiwa kufikiakikomo mwishoni mwa mwaka huu.