Mjumbe wa Bodi ya UTPC Paulina David akizungumza wakati wa kufungua mdahalo wa uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa kwa waandishi wa habari vijana Jijini Mwanza .
Baadhi ya vijana kutoka Chuo cha SAUT Mwanza na waandishi wa habari wakiwa kwenye mdahalo.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza MPC Edwin Soko akitoa mada kwenye mdahalo
************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la kusaidia vyombo vya habari (IMS) wamefanya mdahalo wa uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa kwa vijana na waandishi wa habari vijana.
Mdahalo huo wa siku moja umefanyika leo Jumatatu Novemba 21, 2022 katika Hoteli ya Gold Crest Jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufungua mdahalo huo mjumbe wa Bodi ya UTPC Paulina David, amesema dhumuni kubwa la mdahalo huo ni kuchochea vijana kufahamu umuhimu wa kutoa na kupokea taarifa ikiwa ni sehemu ya haki za msingi za mwanadamu.
Amesema kupitia mdahalo huo vijana watapata nafasi ya kushiriki na kuwa mabalozi wa kuhamasisha masuala yote yanayohusu uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa.
Aidha, David amewaasa vijana kutumia mitandao ya kijamii vizuri wakati wa kutoa taarifa hatua itakayosaidia kuepukana na changamoto ya kuipotosha jamii.
Kwa upande wake Ofisa program mafunzo, utafiti na Machapisho wa UTPC Victor Maleko, amesema UTPC,IMS wamekuwa wakishirikiana kwa karibu katika kuendesha midahalo mbalimbali kwa waandishi wa habari nchini.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko, ni miongoni mwa watoa mada katika mdahalo huo amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu vyombo vya habari vimeimarika kwa kuwa na uhuru wa kuripoti maudhui mbalimbali yenye tija kwa jamii.