Wahifadhi wa Shamba la miti Wino linalomilikiwa na Wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)wakifuatilia mkutano wa wadau wa misitu uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.
……………….
Na Muhidin Amri, Madaba
SERIKALI imewataka wadau wa misitu katika Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma,kuunganisha nguvu zao katika kukabiliana na uharibifu wa misitu ili kuwa na misitu endelevu kwa ajili ya kuharakisha maendeleo na ukuaji wa uchumi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema,wakati akifungua mkutano wa wadau wa misitu na wenye mashamba ya miti jirani na shamba la miti Wino ulioandaliwa na wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS).
Alisema,pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kupitia shamba la miti Wino katika kusaidia kupambana na matukio ya matukio ya moto yanayotokea kwenye mashamba ya miti na misitu ya asili,lakini bado kuna kiwango kikubwa cha uchomaji moto na uharibifu wa mazingira.
Mkuu wa wilaya alisema,uharibifu huo usipodhibitiwa haraka serikali na wadau watalazimika kuingia gharama kubwa ya kurejesha hali nzuri ya mazingira na kusababisha hata kizazi kijacho kushindwa kunufaika na rasilimali za misitu zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Mgema alitoa mfano,mwaka 2021 pekee jumla ya ekta 1,663 za miti katika shamba la Wino zilichomwa moto na watu wasiofahamika na kuitaka jamii inayoishi kuzunguka shamba hilo kuwa walinzi kwani lina mchango mkubwa kiuchumi kwa Halmashauri,mkoa na Taifa.
Amewataka wataalam wa misitu kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji na kata kutoa elimu kwa jamii ya kuanza kutumia nishati mbadala ikiwamo gesi ili kuepusha Halmashauri hiyo kugeuka jangwa kutokana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa yanayofanywa na wananchi.
Katika hatua nyingine Mgema,ameitaka wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS) kupitia shamba la miti Wino kuongeza vifaa vya kuzimia moto ili viweze kutumika pindi moto unapotokea kwenye mashamba ya miti ya kupandwa na asili.
Aidha ameagiza,kuanzia mwezi Januari mwakani kila kaya iwe na shamba la miti kuanzia nusu eka na watu wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kuhakikisha kila mmoja anapanda miti 5 kuzunguka eneo analoishi.
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa shamba la miti Wino Glory Kasmir alisema, TFS kupitia shamba la Wino imejipanga kuongeza kasi ya upandaji miti kutoka ekta 500 za sasa hadi kufikia ekta 3,000 katika maeneo ya Mkongotema na Ifinga Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.
Kasmir alieleza kuwa,malengo ya kuanzishwa kwa hifadhi ya msitu wa Wino ni kuhifadhi maliasili zinazotaka kutoweka ikiwamo vyanzo vya maji,kuzalisha mbao,nguzo za umeme kwa siku za usoni na kutoa ajira kwa wananchi hasa wale wanaotoka katika vijiji jirani.
Amewapongeza wadau wanaojihusisha na upandaji miti,kutokana na mchango mkubwa katika utunzaji mazingira ambapo ameshauri baada ya upandaji wa miti wahakikishe wanahudumia miti hiyo kwa kufanya usafi wa mashamba yao ,kufanya doria na kufungua barabara za ndani na nje ya mashamba.
Mmoja wa wadau wa misitu Dkt Arnold Wella, ameishauri Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii kuanzisha kikosi maalum cha askari ambao kazi yao ni kuzuia matukio ya moto kwenye mashamba ya miti ya kupandwa na misitu ya asili.
Alisema,hatua hiyo itawezesha sana kupunguza matukio ya moto yanayotokea mara kwa mara ambayo yanasababisha hasara kubwa kwa serikali na watu binafsi.