Na Mwandishi wetu, Babati
SHULE ya awali na msingi Tarangire iliyopo mtaa wa Wang’waray Mjini Babati Mkoani Manyara, imezidi kupiga hatua kitaaluma baada ya wanafunzi na walimu kupatiwa tuzo na vyeti.
Mwalimu mkuu wa Tarangire Pre & Primary English Medium School, Juma Ama akizungumza kwenye mahafali ya shule hiyo amesema wanafunzi na walimu hao wamepatiwa tuzo na vyeti hivyo na Serikali.
Mwalimu Ama amesema tuzo hizo na vyeti hivyo vimetolewa Februari 17 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro John Don Twange kutokana na ufaulu bora wa matokeo ya mwaka jana.
Amesema tuzo mbili na vyeti viwili vimetolewa kwa walimu na wanafunzi wa darasa la nne na tuzo tatu na vyeti vitano vya taaluma kwa wanafunzi wa saba kwa mwaka jana.
Amesema shule ya awali na msingi Tarangire imefanikiwa kuongeza wanafunzi kutoka 297 kwa mwaka jana hadi kufikia wanafunzi 330 kwa mwaka huu na pia kushiriki michezo mbalimbali hadi ngazi ya Taifa.
Amesema shule hiyo imekuwa inalipa kodi, imetoa ajira mbalimbali kwa watanzania na kununua vyakula kwa jamii inayowazunguka kama mahindi, mchele, maharage na nyama kwa ajili ya wanafunzi na watumishi wa shule hiyo.
“Shule imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali kwa vitendo kama vile kilimo cha mahindi, ndizi, mbogamboga na ufugaji wa ng’ombe, kuku na mbuzi,” amesema Mwalimu Ama.
Afisa elimu msingi Mji wa Babati, mwalimu Simon Mumbee ameipongeza Tarangire Pre & Primary English Medium School kwa namna inavyojitahidi kutoa taaluma kwa wanafunzi wake.
Mwalimu Mumbee amesema watanzania wanapaswa kupeleka watoto wao katika shule za msingi na sekondari nchini kwani Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha na kuwekeza kwenye elimu kwa asilimia 100.
Askari wa ofisi ya mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Manyara, Mahenda Kera amesema shule ya Tarangire ni wadau wao kwani wamekuwa wakishirikiana na kukumbushana kufanya matengenezo ya mara kwa mara kwenye magari ili watoto wasafiri kwa usalama wakienda shuleni.