Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke akizungumza jambo kwenye kikao cha masheikhe wa mikoa saba ya Kanda ya Ziwa na Magharibi wakiwemo wa wilaya za mkoa huo, kuhusu maandalizi ya Maulidi ya Mtume Muhhamad S.A.W.
Kaimu Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, akifafanua jambo wakati wa kikao cha maandalizi ya kuzaliwa Mtume Muhhamad S.A.W kilichowakutanisha masheikh wa mikoa saba wakiwemo wa wilaya za Mwanza.
Masheikh wa mikoa saba ya Kanda ya Ziwa na Magharibi pamoja na masheikhe wa wilaya za Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa kikao cha maandalizi ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhhamad S.A.W.
******************************
SHEIKH wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta ametoa onyo kwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii ili kuwakatisha tamaa na kuwavunja moyo waumini wa dini ya Kiislamu wasichangie maulidi, waache kufungua mijadala isiyo na tija,badala yake wahamasishe waumini kuchangia sherehe hizo.
Sherehe hizo za Maulid kitaifa zitafanyika jijini Mwanza, Novemba 9, mwaka huu ambapo wageni mbalimbali kutoka nchi jirani za Burundi,Kenya, Uganda watahudhuria.
Sheikh Kichwabuta alita onyo hilo jana baada ya kumalizika kwa kikao cha maandalizi ya sherehe hizo za kuzaliwa kwa Mtume Muhhamad S.A.W kilichofanyika jijini Mwanza na kuwatanisha masheikhe wa mikoa saba ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.
Alisema watu wenye nia mbaya wanatumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kufungua mijadala ya kuwakatisha tamaa na kuwavunja moyo waumini wa dini ya Kiislamu ili wasichangie sherehe hizo wasipewe nafasi.
Sheikhe Kichwabuta, alisema ikibainika kuwa watu wanaotaka kuwarudisha nyuma na kukwamisha shughuli hiyo yenye thawabu ni waislamu wenyewe, basi wasipewe nafasi na wawekwe pembeni hadi mwisho wa maulid hayo.
“Tuhamasishe maulidi ili watu wachangie na tusiweke vitu ama mambo ya kuwavunja moyo waumini.Tusifungue mijadala isiyo na tija kwenye ma-group WhatsApp (makundi) ili kuweza kufanikisha shughuli hii muhimu,”alisema.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Kagera, alishauri kuwa watu wa kuwarudisha nyuma wasipewe nafasi hadi shughuli hiyo iishe ili wasiwavuruge watu wenye fikra nzuri.
Awali Kaimu Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke alisema maulid ya mwaka huu yatafanyika jijini humu ikiwa ni baada ya miaka 40 tangu yafanyike mwaka 1990, yataambatana na shughuli za kijamii ambapo mada mbalimbali zikiwemo za mauaji ya wazee,uhusiano wa watu wa dini zingine na elimu ya dawa zitatolewa.
“Tumekutana hapa kwa ridhaa ya Mufti, Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Bin Zuberi kujadili ili kufanikisha jambo hili la maulid ya kuzaliwa Mtume Muhhamd S.A.W.Wito wangu kwa waislamu na wasio waislamu, ni heshima kwa wanajamii wote kujitokeza kushiriki kwa hali na mali kuchangia na si lazima hadi wafuatwe, wafanye kwa hiari an uungwana wa mtu,”alisema.
Sheikh Kabeke alisema kwenye sherehe hizo kutakuwa na maonyesho ya shughuli za kijamii,zinazofanywa na waumini wa dini ya kiislamu pamoja na kuchangia damu.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Bakwata Mkoa wa Mwanza, Hamis Mwagao, alisema mambo mengi ya kuleta mabdiliko katika sekta za elimu na afya kwa waislamu na jamii yatafanyika hivyo ni fursa pia kwa Watanzania waishio nje ya nchi kuchangia vyakula na fedha za kufanikisha maulidi hiyo hapa kwani wageni kutoka nchi jirani za Burundi,Kenya, Uganda na Rwanda wahudhuria.