Mkuu wa Kitengo cha Mipango Utawala na Rasilimali Watu kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Haji Faki Hamdani akitoa mafunzo kwa mwenyeviti wa kamati za kukabiliana na maafa cha kutathmini hali ya majanga katika shehia za wilaya ya kusini unguja huko katika Ukumbi wa Afisi za Mkuu wa Wilaya Makunduchi kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Elimu Ushauri Nasaha na Tafiti Haji Ame Haji na Mwenyekiti wa Masheha Ali Haji Mkadam wa Bwejuu Dongwe.
Wenyeviti wa kamati za kukabiliana na maafa kutoka katika shehia mbali mbali za Wilaya ya Kusini Unguja wakisikiliza mafunzo kwa Mkuu wa Kitengo cha Mipango, na Rasilimali Watu kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Haji Faki Hamdani ambae hayupo pichani kuhusu jinsi ya kukabiliana na maafa katika shehia zao huko katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Kusini Makunduchi.
Wenyeviti wa kamati za kukabiliana na maafa kutoka katika sheha mbali mbali za Wilaya ya Kusini Unguja wakisikiliza mafunzo kwa Mkuu wa Kitengo cha Elimu Ushauri Nasaha na Tafiti Haji Ame Haji ambae hayupo pichani kuhusu jinsi ya kushirikiana na vyombo vya uokozi wakati wa zoezi la uwokozi pindi maafa yakitokea huko katika ukumbi wa Afisi ya Mkuu wa Wilaya Makunduchi.
*************************************
Na Khadija Khamis- Maelezo Zanzibar 24/09/2019.
Masheha wa Wilaya Kusini Unguja wametakiwa kujua majukumu ambayo yanayowapasa kukabiliana nayo pindipo yakitokea maafa katika shehia zao ili kupunguza adhari zinazoweza kujitokeza .
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Mipango, na Rasilimali Watu kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Haji Faki Hamdani wakati wa kikao cha kutathmini hali ya majanga katika shehia za Wilaya ya Kusini Unguja na Wenyeviti wa kamati ya kukabiliana na maafa
Alieleza kuwa Masheha wa shehia mbao ndio wenyeviti wa kamati ya kukabiliana na maafa iko haja ya kuongoza zoezi la kuondoa au kupunguza viashiria vya majanga katika shehia husika pamoja na kutoa elimu ya kukabiliana na maafa katika shehia zao.
Alifahamisha kuwa masheha waweze kuielimisha jamii njia sahihi za mawasiliano wakati wa dharura inapotokea pia kutenga eneo la makazi wakati wa dharura ndani ya Shehia zao .
Aidha alisema janga ni tukio ambalo linaweza kupelekea maafa na kusababisha adhari kubwa kwa jamii na vilevile maafa ni tukio kubwa ambalo linapelekea adhari ikiwemo vifo na upotevu wa mali .
Mkuu huyo aliwataka masheha kuwa pamoja na jamii hasa kwa wale ambao wamepatwa na majanga ili kuweza kuwafariji pamoja na kushajihisha wengine kwa kuweze kuwasaidia .
“Rasilimali watu ni hazina kubwa kwa maendeleo ya shehia na nchi kiujumla hivyo jamii iweze kuweka tahadhari katika majanga ambayo yanasababishwa na binaadamu “.alisema Mkuu huyo .
Hata hivyo alisema kuna majanga ambayo huwezi kuyaepuka ambayo yanasababishwa na majanga ya kimaumbile ikiwemo kimbunga ,mvua kubwa za mafuriko mtetemeko wa ardhi na mengineyo hayo husababisha vifo na upotevu wa mali kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi .
Nae Mkuu wa Kitengo cha Elimu Ushauri Nasaha na Tafiti Haji Ame Haji amewataka wenyeviti hao kuratibu ufanyaji wa tathmini ya awali juu ya athari iliyojitokeza baada ya maafa na ripoti iwasilishwe kwa wahusika pamoja na kufahamisha aina ya mahitaji wanayohitajia wahanga .
Vilevile mkuu wa kitengo cha elimu huyo aliwataka wenyeviti hao kutunza kumbukumbu za matukio ya majanga yanayotokea katika shehia zao ili kusaidia kurejesha hali kulingana na uwezo wao.
Kwa upande wa wenyeviti hao wamesema kuwa wanakazi kubwa kuielewesha jamii kwani wananchi hawajui majanga wala ajali wanachotaka wao wafanye wapendalo .
Wenyeviti hao waliiyomba Serikali za Halmashauri kufika katika maeneo ya shehia zao ili kuona hali halisi ya mpango miji inayojengwa na kuweza kutoa ushauri kwa wananchi .
Wenyeviti hao walisema kuwa Sheha ni jina kubwa lakini halina kitu hivyo wakati mwengine hupata wakati mgumu kwa jamii ambapo huwa ni tegemeo lao kubwa la kupata kupewa mkono wa pole .