Home Mchanganyiko UBA yatimiza ahadi ya nyumba kwa pacha waliotenganishwa Muhimbili

UBA yatimiza ahadi ya nyumba kwa pacha waliotenganishwa Muhimbili

0

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh. Jokate Mwegelo (kulia) na Mkurugenzi wa UBA Bw. Usman Isiaka wakizindua nyumba kwa ajili ya makazi ya pacha Pracious na Gracious waliozaliwa wakiwa wameungana na baadaye kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha MNH.

Mh. Jokate Mwegelo akifurahia mandhari ya ndani ya nyumba hiyo, kushoto kwake ni Balozi wa Sherisheri nchini Mh. Maryvonne Pool.

Mh.Jokate Mwegelo akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa UBA Usman Isiaka akizungumza wakati wa hafla hiyo.

********************************

United Bank for Africa (UBA) imetimiza ahadi yake ya kuwajengea nyumba ya kisasa watoto pacha Precious na Gracious Mkono waliozaliwa Julai, 2018 wakiwa wameungana na baadaye kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa tarehe 23 Septemba, 2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).  

                                                                                                                         

Nyumba hiyo imejengwa katika Kata ya Mzenga, Wilaya ya Kisarawe ambapo awali mapacha hawa walikuwa wakiishi katika makazi duni kwenye Kata ya Kimaramsele.

                                                                                                                         

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyumba hiyo iliyofanyika leo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mh. Jokate Mwegelo amesema kuwa walipata moyo wa kutafuta wafadhili kwa ajili ya kusaidia mapacha hao baada ya upasuaji wao na wa kihistoria kufanyika kwa mafanikio na hivyo kuhitajika waishi kwenye makazi salama ambapo huduma muhimu za kijamii zinapatikana.

 

Amesema aina ya upasuaji wa kuwatenganisha uliofanywa na MNH ulikuwa wa kihistoria kwa taifa letu na mara ya mwisho wataalamu hawa walifanya upasuaji wa aina hiyo miaka 25 iliyopita.

 

“Tunataka watu wajue kuwa Muhimbili ya sasa si ile ya zamani, sasa hivi chini ya utawala wa Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli tunao wataalamu wanaoweza kufanya upasuaji wa namna hii na tunaomba dunia ijue hili” amesema Mh. Mwegelo

 

Pia Mh. Mwegelo amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru kulipia gharama za upasuaji wa watoto hao uliogharimu Tshs.  34 milioni ambazo zililipwa na Hospitali.

 

Aidha Mh. Mwegelo ameishukuru UBA kugharamia ujenzi wa nyumba hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 18, ambapo ujenzi wake umetumia siku 28 hadi kukamilika na pia amemshukuru Balozi wa visiwa vya Sherisheri nchini Mh. Maryvonne Pool kulipia gharama za ununuzi wa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UBA Bw.Usman Isiaka amesema kuwa walipopata habari za upasuaji huo wa kihistoria uliofanyika MNH waliguswa na waliamua kuwatafutia watoto hao bima ya afya, kuwafungulia akaunti kwa ajili kuwawekea fedha  takribani Tshs. 2 milioni kama kianzio cha maisha pamoja na kuwajengea nyumba ya kuishi ambayo ni salama kwa ustawi wa afya zao.

 

Daktari Bingwa na Mshauri Mwelekezi wa Upasuaji wa Watoto MNH Dkt. Petronila Ngiloi ambaye alishiriki kufanya upasuaji wa kutenganisha mapacha hao amesema kuwa amefurahi kuona watoto hao wamepata sehemu salama ya kuishi kwani baada ya kuwafanyia upasuaji changamoto iliyojitokeza ilikuwa ni makazi bora kwa ajili ya malezi salama ya watoto hao kwani ilibainika kuwa wanatoka katika makazi duni.