Na mwandishi wetu,Dar es salaam.
Ikiwa leo Taifa la Tanzania linakumbuka miaka 23 tangu kufariki Kwa aliekuwa Rais wa kwanza Hayati Mwalimu *Julius Kambarage Nyerere* Kinyozi maarufu hapa nchini ambaye pia ni mfanyabiashara wa saluni Rejay Juma alimaarufu Kama ‘cutting master’ leo ametoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo vyakula Kwa akina mama wanaoishi mazingira magumu ya kuponda mawe katika eneo la Mbuyuni, kunduchi manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam.
Akizungumza mara baada ya kutoa msaada huo Rejay amesema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kuwaunga mkono wanawake hao Kwa kile kidogo ambacho amejaaliwa na Mwenyezi Mungu Kwa kurudisha katika jamii ya watu wanaoishi katika mazingira magumu ya utafutaji wa riziki za kila siku.
Amesema yeye kama kijana anaamini bado Kuna uhitaji mkubwa wa misaada katika jamii ya watu wanaoishi mazingira magumu hasa wanawake ambao huponda mawe katika eneo hilo ili kupata kokoto ambazo baadaye huziuza na kupata hela kidogo ambazo zinawakwamua Kwa kiasi katika maisha.
Katika msaada huo kinyozi huyo maarufu hapa nchini ‘cutting Master’ ametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo sabuni, mafuta ya kupikia, Mchele, Sukari pamoja na nguo huku akiwaasa watanzania kuwa na utamaduni wa kutoa misaada Kwa watu wenye uhitaji na wanaofanya kazi katika mazingira magumu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“nawashauri vijana wenzangu ambao mtaguswa kwa namna moja au nyingine kuwatembelea wanawake hawa na kuwapa misaada ya hali na Mali au hata kuwatembelea watu wengine kama hawa popote pale na kuwapa misaada kwani kufanya hivi kutawapunguzia makali ya maisha” alisema.
Kwa upande wao baadhi ya wanawake waliopewa msaada huo wamemshukuru Kwa msaada huo Kwa kusema kuwa utawapunguzia makali ya maisha kwani kazi wanazofanya (kuponda mawe) ni ngumu ambapo huzifanya juani na kupata fedha kidogo kuanzia shilingi elfu tatu mpaka elfu tatu na mia tano Kwa siku huku kiasi hicho cha pesa kikiwa hakitoshelezi mahitaji yao
Bi Metilda Masini ni Mmoja ya wanawake hao waponda mawe katika eneo la Mbuyuni, kunduchi ambaye amesema amefarijika kupata msaada huo huku akiiomba serikali na wadau wengine wenye mapenzi mema kuwatembelea na kujionea ugumu wa kazi wanazofanya na hatimaye kuiomba serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais *Samia Suluhu Hassan* kuwapatia mikopo ambayo itawawezesha kubadili biashara Kwa kufanya biashara nyingine ambazo zitawaingizia kipato na kuwasaidia katika kuendesha maisha yao kwani wanazofanya Kwa sasa ni ngumu mno na wanaifanya Katika mazingira magumu.