**********************
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa mbio za hiari za Mwl. Nyerere Marathon zitakazofanyika Oktoba 1,2022 Wilayani Butiama Mkoa wa Mara.
Akizungumzia Mbio hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga amesema, uzinduzi wa mbio hizo ni sehemu ya kuenzi, kutangaza na kuhifadhi historia adhimu na adimu ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere.
“Mbio hizi zinajulikana kama Mwl Nyerere Marathon, zinahusisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi na washiriki wa mbio hizi watakimbia kupitia njia alizotumia Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere kwenda Shule na shughuli zake za kila siku akiwa Butiama” Amesema Dkt. Lwoga.
Dkt. Lwoga ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kuungana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana kwenye mbio hizo ili kumuenzi muasisi wa Taifa la Tanzania kwa vitendo.
Aidha, amesema kuwa mbio hizo zimegawanyika katika makundi yatakayohusisha wakimbiaji wa Kilomita 22, 13 na Kilomita 4 inayowakilisha tarehe mwezi na mwaka aliozaliwa Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere.