Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es salaam Elihuruma Mabelya akizungumza na waandishi wa habari akielezea mafanikio ya Manispaa ya hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,utoaji wa huduma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na mikakati kwa mwaka wa fedha 2022/2023.Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es salaam Elihuruma Mabelya (kulia) Pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Manispaa ya Temeke Francisca Mselemo (kushoto) wakati wa kikao na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ambao wamehudhuria Katika mkutano wa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Pamoja na waandishi wa habari.
………………………
NA MUSSA KHALID
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Mkoani Dar es salaam imepanga kukusanya kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bill 43 ikiwa ni mkakati wa kuimarisha na kukuza kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Elihuruma Mabelya wakati akizungumzia mafanikio ya Manispaa ya Temeke katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,utoaji wa huduma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na mikakati kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mabelya amesema kuwa Halmashauri hiyo imeendelea kufanya vyema katika ukusanyaji wa mapato kwani kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 imefanikiwa kukusanya Jumla ya Tsh Bill 39.9 sawa ma asilimia 106 na hivyo kuvunka lengo kwa asilimia 6.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 watahakikisha wanakusanya Bill 43.3 kwani mafanikio ya kitaasisi ni jambo endelevu hivyo malengo yao nikuendelea kuyapata mafanikio na kuwa Manispaa ya mfano nchini.
“Mikakati ya Manispaa Katika kuimarisha na kukuza kiwango Cha ukusanyaji wa mapato Kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 ni Pamoja na kutoa elimu ya juu ya Umuhimu wa kulipa ushuru na ada mbalimbali kwa Maendeleo ya Wilaya na Taifa,lakini pia kuimarisha ukaguzi wanaokwepa kulipa ushuru na ada Kwa hiari na wanaovunja sheria ndogo”amesema Mabelya
Aidha kuhusu Idara ya Elimu Sekondari amesema Manispaa imefanikiwa kutekeleza Miradi mbalimbali yenye thamani ya Shilingi Bill 4.8 ambayo ni Ujenzi wa vyumba vya madarasa 175,bweni 1,bwalo 1,matundu ya vyoo 90,maabara 12,Shule Mpya 1 (Dovya Sekondari) Pamoja na mradi wa miundombinu ya maji.
Mkurugenzi Huyo ameendelea kusema kuwa katika Idara ya Elimu Msingi Manispaa Kwa kupitia mapato yake ya Ndani imefanikiwa kutekeleza Ujenzi wa vyumba vya madarasa 1598,matundu ya vyoo 1797,Ununuzi wa madawati 37, ambapo thamani ya miradi hiyo ni Shilingi Bill 1.4.
Kuhusu Idara ya maendeleo ya jamii na vijana,Mabelya amesema Halmashauri imefanikiwa kutenga kiasi cha Shilingi Bill 3 kwa ajili ya utoaji wa mikopo ambapo mpaka kufika mwezi Juni 2022 wamefanikiwa kutoa Tshs Bill 3 kwa ajili ya kukopesha vikundi.
Hata hivyo Mkurugenzi Huyo ameendelea kuwasisitiza watumishi wa Manispaa hiyo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili waendelee kufanikisha kwa wakati miradi mbalimbali ya kimkakati waliyoipanga.