Mratibu THRDC – Zanzibar, Abdallah Abeid (wa pili kulia) pamoja na Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Khamis Bakar Hamis (wa tatu kushoto ) wakisaini hati ya makubaliano baina ya THRDC na Chuo cha Mafunzo Zanzibar.Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Khamis Bakar Hamis akizungumza baada ya utiaji saini hati ya mashirikiano na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kupitia tawi lake la Zanzibar (THRDC-Zanzibar)Mratibu Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kupitia tawi lake la Zanzibar (THRDC-Zanzibar), Abdallah Abeid akizungumza baada ya utiaji saini hati ya mashirikiano na Chuo cha Mafunzo Zanzibar.Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC – Onesmo Olengurumwa akizungumza mara baada kushuhudia utiaji saini hati hiyo wa mashirikiano baina ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kupitia tawi lake la Zanzibar (THRDC-Zanzibar), na Chuo cha Mafunzo Zanzibar
………………………
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kupitia tawi lake la Zanzibar (THRDC-Zanzibar), hii leo umesaini hati ya makubaliano (MoU) baina yake na Chuo cha Mafunzo Zanzibar kwa lengo la kurasimisha mashirikiano baina ya Chuo na Mtandao hasa katika kuboresha mifumo ya usimamizi wa Haki za Binadamu katika Vyuo vya Mafunzo Visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa Taarifa ambayo imetolewa leo Afisa Habari THRDC imesema tukio hilo la utiwaji saini hati ya makubaliano baina ya THRDC na Chuo cha Mafunzo Zanzibar, limeshuhudiwa na Kamishina wa Chuo cha Mafunzo, Khamis Bakari Khamis, Naibu Kamishna, Haji Hamdu Omar, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Daudi Antony Luswaga, Mkuu wa Idara ya Sheria na Urekebishaji SSP, Seif Makungu pamoja na Maofisa waandamizi na Maofisa wadogo kutoka chuo cha Mafunzo.
Kwa upande wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Bianadamu Tanzania zoezi hili limeshuhudiwa na Mratibu wa THRDC-Zanzibar, Bw. Abdalla Abeid, Mratibu Kitaifa THRDC – Onesmo Olengurumwa, Afisa Programu wa THRDC-Zanzibar Bi. Shadida Omar pamoja na maofisa wengine wa Mtandao, Waandishi wa Habari kutoka katika vyombo mbali mbali vya habari nchini.
Akizungumza baada ya utiaji saini hati hiyo wa mashirikiano Mratibu THRDC – Zanzibar, Abdallah Abeid ameushukuru uongozi wa Chuo cha Mafunzo kwa kuona umuhimu wa kurasimisha mashirikiano yake na THRDC, mashirikiano ambayo yamelenga maeneo mbali mbali ikiwemo;
1) Kuendesha shughuli za kujenga uwezo kwa maofisa wa vyuo vya mafunzo.
2) Kuendesha mafunzo rejea na warsha na mafunzo mbali mbali ya Haki za Binadamu kwa Maofisa wa Chuo cha Mafunzo (ZIEO).
3) Kufanya tafiti na kuchapisha nyenzo muhimu kwa ajili ya uboreshaji wa hali ya vituo vya kurekebisha tabia na haki za binadamu kwa wanafunzi (Wafungwa) Zanzibar.
4) Uboreshaji wa huduma zinazotolewa kwa wafungwa na miundombinu ya vituo vya kurekebisha tabia Zanzibar.
5) Mashirikiano katika eneo lingine lolote muhimu la mashirikiano linaloweza kutambuliwa katika siku zijazo kulingana na mahitaji.
6) Kubuni na kuunga mkono mipango ya marekebisho ya sheria na sera mbali mbali za Vyuo vya Mafunzo Zanzibar.
“Kwa Upande wa Chuo cha Mafunzo tumeanza na utengenezaji wa mwongozo ambao utasaidia kaukusanyaji wa taarifa zinazohusiana na uvunjifu wa haki za binadamu katika vyuo vya mafunzo lakini katika mchakato wa utpitiaji wa sheria tulianza juzi na Watendaji mbali mbali wa aAsasi za kiraia na wao wametoa maoni yao, na leo tuna maofisa wa chuo cha mafunzo takribani 15 na wao watapata fursa ya kujadili sheria hiyo kwa ajili ya kuboresha zaidi, haya ni baadhi tu ya mambo mengi ambayo tunaendelea kushirikiana na Chuo cha Mafunzo, hivyo tunasaini MOU hii kwa kuwa maofisa wa Chuo cha mafunzo nao pia ni Watetezi wa Haki za binadamu” Abdalla Abeid, Mratibu THRDC- Zanzibar
Kwa upande wake Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Khamis Bakar Hamis ameeleza mashirikiano waliyoingia na Mtandao katika kuendeleza haki za binadamu kwa Wanafunzi pindi wawapo vizuizini.
“Katika makubaliano haya ndani ya vyuo vya mafunzo kuna swala la haki za binadamu, Mwanafunzi anapokuja chuo cha mafunzo ingawa ni mkosefu wa sheria au amefanya makosa huko nje, akifika chuoni atatendewa kwa mujibu wa sheria na Haki za binadamu. Yupo ndani lakini bado Haki za msingi za Binadamu zinatakiwa kuendelezwa, kwa hiyo THRDC watashirikiana na sisi (Chuo cha mafunzo) katika makubaliano ya leo kuendeleza haki za binadamu na hasa kwa ambao watakuwa ndani. Tupo tayari kufanya yote tutakayokubaliana leo, tunaomba na ninyi mfanye kwa upande wenu ili kwa pamoja tusimamie haki za binadamu kwa wanafunzi waliopo vuzuizini kwa kufuata miongozo ya nchi na kwa mujibu wa taratibu za kimataifa.” Khamis Bakari Khamis, Kamishina wa Chuo cha Mafunzo.
Pamoja na utiaji sahihi makubaliano hayo ya mashirikiano na Chuo cha Mafunzo, THRDC kwa kushirikiana na Chuo hicho inaadaa mwongozo wa utoaji wa malalamiko kwa wanafunzi (Wafungwa) pindi wawapo vizuizini, Upitiaji wa Sheria ya kufuta sheria ya Chuo cha Mafunzo Namba 1 ya mwaka 1980 na Namba 3 ya mwaka 2007 ili kuanzisha sheria mpya kwa hatua ya awali, pamoja na mapendekezo ya Sera ya Chuo cha Mafunzo yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Tangu kuanzishwa kwake THRDC- Zanzibar imefanikiwa kusaini makubaliano ya Mashirikiano na taasisi mbili visiwani Zanzibar ikiwemo Mahakama (Mwishoni mwa Mwaka 2021) pamoja na Chuo cha Mafunzo, makubalinao yaliyosainiwa mapema leo, Septemba 28, 2022. Hii yote ni katika kuhakikisha mtandao unarasimisha mashirikiano baina yake na taasisi hizo hasa katika uboreshaji wa huduma zinazotolewa ili zitolewe kwa kufuata misingi ya Haki za binadamu.